CHARLES WASONGA: Kenya na Somalia ziimarishe vita dhidi ya kundi la kigaidi

CHARLES WASONGA: Kenya na Somalia ziimarishe vita dhidi ya kundi la kigaidi

NA CHARLES WASONGA

KENYA na Somalia zinapaswa kuimarisha vita dhidi ya kundi la Al Shabaab wakati ambapo taifa hilo jirani limebuni serikali mpya baada ya kuchaguliwa kwa Rais Hassan Sheikh Mohamud Mei 2022.

Juzi, Rais Mohamud alifanya ziara ya siku mbili nchini ambapo yeye na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta walitia saini mkataba wa ushirikiano katika nyanja mbalimbali ikiwemo vita dhidi ya ugaidi.

Lakini wiki moja baada ya ziara hiyo, wafuasi wa Al Shabaab walivamia msafara wa polisi wa Kenya katika kaunti ndogo ya Elwak, Kaunti ya Mandera na kuwajeruhi saba kati ya maafisa hao.

Hii ina maana kuwa ipo haja kwa serikali za Kenya na Somalia kuanzisha operesheni kali dhidi ya magaidi hao kulingana na makubaliano katika mkataba huo.

Kufunguliwa kwa mpaka wa mataifa hayo mawili, katika sehemu ya Mandera kwa ajili ya kufufua biashara kwa manufaa wakazi wa maeneo hayo ya mpakani, hakutakuwa na faida yoyote, endapo magaidi hawa hawatatokomezwa kabisa.

Hii ni kwa sababu, magaidi hao watatumia mwanya huo kuingia nchini Kenya kwa urahisi na kutekeleza mashambulio.

Hali hiyo pia itawaogofya wasafirishaji wa miraa na bidhaa nyinginezo kutoka Kenya, kupelekwa katika masoko ya Somalia.

Rais Mohamud alitangaza kuondolewa kwa marufuku iliyowekwa na mtangulizi wake Somalia, Mohamed Abdullahi Mohamed, almaarufu Farmajoo, dhidi ya miraa kutoka Kenya, mnamo 2019.

Kwa hivyo, ili Kenya na Somalia zifaidi kutokana na kuondolewa kwa marufuku hii, maafisa wa usalama hawana budi kuendelea kuwaandama magaidi wa Al Shabaab.

Aidha, raia wa mataifa hayo mawili ambao huwasaidia wapiganaji hao kutekeleza , wanafaa kuandamwa na kuadhibiwa kwani wao ni sawa na magaidi.Wakenya hawajasahau shambulio lililotekelezwa na wapiganaji hao wa Al Shabaab katika Chuo Kikuu cha Garissa mnamo Aprili 2, 2015, ambapo watu 148 waliuawa, wengi wao wakiwa wanafunzi.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Kenya yajikokota kusaka fidia kwa familia...

Ujumlishaji kura Kieni waendelea IEBC ikitarajia shughuli...

T L