CHARLES WASONGA: Kuzimwa kwa mawaziri wanaoondoka kutazuia matumizi mabovu ya mamlaka

CHARLES WASONGA: Kuzimwa kwa mawaziri wanaoondoka kutazuia matumizi mabovu ya mamlaka

NA CHARLES WASONGA

RAIS William Ruto ametoa amri ya busara zaidi kwa kuwazima mawaziri wanaoondoka kufanya teuzi mbalimbali za umma, kutoa zabuni kubwa katika wizara zao na hata kufanya safari za ng’ambo.

Agizo hilo linafaa hasa wakati huu wa mpito kutoka utawala wa rais mstaafu Uhuru Kenyatta hadi huu mpya wa Dkt Ruto kwani itaziba mianya ya wizi na ubadhirifu wa pesa za umma.

Historia ya nchini hii imeonyesha kuwa sakata nyingi hutokea katika kipindi kama hicho cha mpito kutoka utawala mmoja hadi mwingine.

Mifano hapa ni sakata ya Goldenberg iliyotokea kuelekea uchaguzi mkuu wa 1992 na ile ya Anglo Leasing iliyochupika muda mfupi tu baada ya Rais mstaafu Mwai Kibaki kuingia mamlakani mnamo Desemba 30, 2002.

Isitoshe, mnamo Aprili 2022, Afisa Mkuu wa Tume ya Kupambana na Ufisadi (EACC) Twalib Mbarak alisema uchuguzi wa afisi yake umebaini kuwa maafisa wengi wa serikali hushiriki maovu nyakati za mpito.

Aghalabu maovu hayo, hasa hutokea katika shughuli za utoaji zabuni, uajiri au uteuzi wa maafisa katika idara na mashirika mbali mbali.

Hii ni kwa sababu baadhi ya maafisa wahusika hususan mawaziri, makatibu wa wizara na wakuu wengine huongozwa na tamaa ya kujipatia fedha za haraka baada ya kung’amua kuwa watatemwa na utawala mpya.

Kwa hivyo, hatua ambayo Rais Ruto alichukua itasaidia kuzima tabia kama hizo za maafisa kutumia njia za mkato kujilimbikizia mali au kutumia mamlaka ya afisi zao kuwatunuku marafiki wao kwa kuwateua haswa kati mashirika ya serikali.

Licha ya kuwa kuna baadhi ya mawaziri na makatibu wao ambao walimkwaza Dkt Ruto wakati wa kampeni kwa kutumia mamlaka ya afisi zao kuhangaisha wandani, ninaamini kuwa hatua hii ya kudhibiti mamlaka yao sio kitendo cha ulipishaji kisasi.

Lakini kile ambacho Rais Ruto alifanya, na ambacho kilikuwa kinyume na utaratibu rasmi serikalini, ni kutoandamana na Waziri wa Masuala ya Kigeni anayeondoka Rachel Omamo na Katibu wake, Macharia Kamau, katika ziara yake nchini Uingereza na Amerika.

Badala yake, Rais akiandamana na idadi kubwa ya wanasiasa wandani wake, na washirika wake wengine katika muungano wa Kenya Kwanza, ambao kufikia sasa hawashikilii wadhifa wowote serikalini.

  • Tags

You can share this post!

Hofu Ebola ikichacha Uganda

Kibarua kwa Ruto kutuliza ulafi bungeni

T L