CHARLES WASONGA: Mpango wa kuwapa machifu bunduki utekelezwe kisheria

CHARLES WASONGA: Mpango wa kuwapa machifu bunduki utekelezwe kisheria

NA CHARLES WASONGA

UTAWALA wa mkoa ulikuwa kiungo muhimu zaidi katika tawala zilizopita za Hayati Mzee Jomo Kenyatta, Daniel arap Moi na Mwai Kibaki.

Maafisa wa utawala wa mkoa kuanzia ngazi za mkoa (waliokuwa wakuu wa mikoa) hadi kata ndogo zinazosimamiwa na manaibu wa chifu ndio waliokuwa macho na masikio ya rais.

Miongoni mwa majukumu yao yalikuwa (na yangali) kudumisha sheria na usalama, kufafanua sera za serikali katika maeneo wanayosimamia.

Kabla ya mamlaka ya maafisa hawa kupunguzwa baada ya Kenya kupata Katiba mpya ya 2010, walikuwa na nguvu nyingi mno.

Hii ndiyo maana baadhi yao walitumia nguvu hayo vibaya kwa kuwahangaisha na kuwadhulumu wananchi.

Ndiposa wakati wa shinizo za mageuzi ya katiba ziliposhika kasi kuanzia mapema miaka ya ‘90, Wakenya walipendekeza utawala wa mkoa uondolewe au ufanyiwe marekebisho sambamba na asasi ya urais na idara ya polisi.

Asasi hizi zilionekana kuendeleza utawala wa kidikteta na vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu.

Lakini hata baada ya ujio wa katiba ya sasa, kubadilisha mfumo wa zamani wa utawala kwa kuondoa ngazi za utawala kama vile mikoa, wilaya na tarafa, serikali ya rais mstaafu Uhuru Kenyatta ilirejesha mfumo huo wa zamani kupiti Sheria ya Ushirikishi wa Majukumu ya Serikali ya Kitaifa ya 2013.

Sheria hii ilidumisha machifu lakini ikaondoa nyadhifa za Wakuu wa Mikoa (PC), Wakuu wa Wilaya (DC) na Wakuu wa Tarafa (DO).

Lakini sheria hiyo ilibuni nyadhifa za Washirikishi wa Kanda, Makamishna wa Kaunti na Manaibu wa Makamishna wa Kaunti, ambao pamoja na machifu wameendelea kuwa wawakilishi wa Serikali Kuu kuanzia ngazi ya kitaifa hadi mashinani.

Japo utawala wa mikoa ulifanyiwa mageuzi huku Sheria dhalimu ya Machifu (Chiefs Administration Act) ikiondolewa, bado kuna manung’uniko ya matumizi mabaya ya maafisa hawa wa utawala, hususan machifu. Mathalan, katika uchaguzi mkuu wa 2017, upinzani uliilaumu serikali ya Jubilee kwa kutumia machifu kufanikisha kampeni zake.

Mrengo wa Kenya Kwanza ulitoa madai sawa na hayo kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kwa kudai machifu walikuwa wakitumiwa na mrengo wa Azimio la Umoja-One Kenya kutisha wafuasi wake wasijitokeze kupiga kura.

Ni kwa msingi huu ambapo mpango wa Waziri wa Usalama, Prof Kithure Kindiki, kuwapa machifu na manaibu wake bunduki na polisi wa kuwalinda tayari umeibua wasiwasi kuwa serikali inalenga kurejesha mfumo dhalimu wa zamani wa utawala.

Kulingana na Prof Kindiki, machifu watakaopewa bunduki ni wale wanaohudumu katika maeneo ambako visa vya utovu wa usalama vimekithiri zaidi kama vile Kaskazini mwa Bonde la Ufa na Kaskazini Mashariki.

Japo wazo hili ni zuri ikizingatiwa kuwa machifu wengi wameauawa na wahalifu katika maeneo hayo, utekelezaji wa mpango huo unapasa kutangulizwa na majadiliano ya kina kabla ya kutekelezwa.

Wizara ya Usalama wa Ndani inapaswa kuandaa vikao vya kukusanya maoni kutoka kwa umma na wadau wengine kuhusu mpango huo kisha ibuni kanuni za kuongoza utakelezaji wa mpango huo.

Kipengele cha 118 cha Katiba ya sasa kinasema kuwa ni lazima serikali ishirikishe maoni ya umma kwanza kabla ya kutekeleza sera au mpango wowote utakaoathiri wananchi hao.

Kanuni zitakazoongoza mpango huo wa kuwapa machifu bunduki pia zijadiliwe na umma na wabunge kabla ya kutekelezwa.

  • Tags

You can share this post!

BENSON MATHEKA: Usalama wa kila mtahiniwa uhakikishwe...

Watahiniwa wahamishwa kwa ndege ya KDF msituni Boni

T L