CHARLES WASONGA: Museveni amesaidia Uganda licha ya utawala wake wa kiimla

CHARLES WASONGA: Museveni amesaidia Uganda licha ya utawala wake wa kiimla

Na CHARLES WASONGA

INGAWA ni kweli kwamba Rais Yoweri Museveni ameongoza Uganda kwa udikteta kwa zaidi ya miongo mitatu, nchi hiyo jirani imefurahia kiwango fulani cha utulivu chini ya kiongozi huyo mkongwe.

Tofauti na enzi za marais wa zamani wa Uganda kama vile Idi Amin na Milton Obote, Museveni amefaulu kujenga uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hiyo na mataifa jirani ya Afrika Mashariki, Afrika na Ulimwengu kwa ujumla.

Isitoshe, chini ya uongozi wa Museveni, Uganda imekuwa mshirika mkubwa katika shughuli za Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Shirika la Maendeleo katika kanda hii (IGAD).

Muhimu zaidi kwetu kama Wakenya ni kwamba chini ya uongozi wa Museveni, biashara kati ya Kenya na Uganda imenawiri zaidi kuliko ilivyokuwa chini ya tawala za hapo nyuma.

Wakenya wengi pia wanasoma katika vyuo vikuu nchini Uganda huku wengine wakiendesha biashara jijini Kampala na miji mingine mikubwa.

Kulingana na takwimu zilizotolewa kwenye ripoti ya hali ya uchumi nchini mwaka jana, 2020 (Economic Survey, 2020) Kenya iliuza bidhaa za thamani ya Sh64.1 bilioni nchini Uganda mnamo mwaka wa 2019.

Uganda nayo iliuza bidhaa za thamani ya Sh43 bilioni nchini Kenya, ishara tosha kwamba Kenya imekuwa ikifaidi zaidi katika biashara kati yake na taifa hili jirani.

Hii ina maana kuwa Kenya itaendelea kufaidi zaidi kibiashara kufuatia kuchaguliwa tena kwa Rais Museveni katika uchaguzi uliokamilika wiki jana, licha ya madai ya wizi wa kura yaliyoibuliwa na mgombeaji wa upinzani Robert Kyangulanyi.

Isitoshe, hii ndio sababu serikali ya Kenya, sawa na vyombo vya habari nchini, itakuwa ikifuatilia kwa makini hali nchini Uganda baada ya uchaguzi huo kwa matumaini kwamba amani itaendelea kudumu.

Sasa ni wajibu wa Rais Museveni kuhakikisha kuwa amani imedumu nchini humo ili aweze kutekeleza ajenda zake za maendeleo katika nyanja ya elimu, afya na kilimo, alivyosema katika hotuba yake kwa taifa saa chache baada ya kutangazwa mshindi Jumamosi.

Akome kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya viongozi wa upinzani, wafuasi wao, wanahabari na wakosoaji wake wengine alivyofanya kabla na wakati wa uchaguzi huo wa Januari 14.

Kama mmoja wa marais wakongwe zaidi barani Afrika, Museveni sasa anafaa kubadili mtindo wake wa uongozi kwa kukomesha vitendo vya udhalimu ili uongozi wake uweze kuwa wenye manufaa zaidi kwa raia wa Uganda na wale wa mataifa jirani.

You can share this post!

FAUSTINE NGILA: Madikteta wasiruhusiwe kutumia mitandao...

WANDERI KAMAU: Jamii imefeli ila ijikakamue kuelekeza...