CHARLES WASONGA: Raia wanabaguliwa katika utekelezaji sheria za corona

CHARLES WASONGA: Raia wanabaguliwa katika utekelezaji sheria za corona

Na CHARLES WASONGA

NAKUBALIANA na kauli ya maafisa wa afya katika kaunti ya Nairobi kwamba wanasiasa ndio wanachochea ongezeko la visa vya maambukizi ya Covid-19 kwa kukiuka masharti ya kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huu hatari.

Katika siku za hivi karibuni, kaunti za Nairobi na Kiambu zimeandikisha ongezeko la visa vya maambukizi mapya kutokana na kampeni za kisiasa zilizoendeshwa na wanasiasa kuelekea chaguzi ndogo za eneo bunge la Kiambaa na wadi ya Maguga.

Ingawa, mnamo Mei 30 serikali ilipiga marufuku mikutano ya hadhara ya kisiasa kwa muda wa siku 60 zaidi, wanasiasa wa vyama na mirego yote wamekuwa wamekaidi marufuku hiyo; ilivyodhihirika katika changuzi hizo zilizokamilisha juzi.

Hii ni dhihirisho kwamba wanasiasa wetu, wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, huwa hawajifunzi kutokana na makosa yao ya siku za nyuma.

Inakumbukwa kwamba ukaidi huu wa wanasiasa ndio ulichangia ongezeko la maambukizi ya corona katika kaunti za Nyanza na Magharibi.

Visa viliongezeka katika maeneo hayo baada ya sherehe za kitaifa za Madaraka Dei kuandaliwa jijini Kisumu ambapo wanasiasa waliwahutubia wananchi na kuchochea msambao wa aina ya virusi vya corona ijulikanayo kama, Delta.

Baadaye serikali iliweka masharti zaidi ya kuzuia maambukizi kwa kuongeza muda wa kafyu na kufunga masoko ya wazi, hali iliyowaumiza zaidi raia wa kawaida.

Isitoshe, hivi majuzi kiwango cha maambukizi kilipanda katika kaunti ya Nakuru baada ya mbio za dunia za magari almaarufu, Safari Rally kuandaliwa katika eneo la Naivasha.

Kwa hivyo, inavunja moyo huku wananchi wa kawaida wakiendelea kushurutishwa kuzingatia masharti ya kudhibiti janga la corona, huku serikali ikikosa kufanya chochote kuwaadhibiti wanasiasa wanaokiuka masharti yayo hayo.

Hii ni licha ya wanasayansi kuonya kwamba kwamba Kenya iko hatari ya kuathiriwa na mlipuko wa wimbi la nne la maambukizi ya corona.Ingawa, kwa ujumla, idadi ya maambukizi ambayo yananakiliwa nchini ni ndogo ikilinganishwa na ya mapema mwaka huu.

Kenya ingali ni miongoni mwa mataifa 10 barani Afrika ambayo yanaandikisha idadi za juu za maambukizi na vifo kutokana na gonjwa hili hatari.

Kwa hivyo, serikali inapaswa kuendelea kukaza kamba kwa kuhakikisha masharti yote ya kuzuia msambao wa corona yanazingatiwa na wananchi wote bila kuzingatia matabaka yao.

Kwa mfano, hamna haja ya wanasiasa kuhuruhusiwa kuhutubia mikutano ya hadhara baada ya kuhudhuria ibada za Jumapili katika makanisa mbalimbali nchini.

Wale wanaendeleza mtindo huu, hatari kwa maisha, ni Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi.Kila Jumapili utawapata wawili hawa wakihutubia mikutano nje ya makanisa bila kujali kwamba hiyo ni mojawapo ya njia kuu za kueneza virusi vya corona.

Kinachoudhi hata zaidi ni kwamba kando na kukaidi kanuni ya kutokaribiana, wanaokongamana kuwasikiliza wanasiasa hao huwa hawavalii barakoa au huzivalia visivyo.

Juzi, kiongozi wa ODM Raila Odinga, naye alihutubia mkutano wa hadhara alipofanya kwenye ziara katika kaunti ya Tana River, akisahau kuwa amewahi kuwa mwathiriwa wa Covid-19.

Ikiwa serikali imeshindwa kuwachukulia hatua wanasiasa wanaovunja masharti ya kuzuia kuenea kwa janga hili, basi iondoe ya masharti yanayowaumiza raia kiuchumi, kama vile kafyu na magari ya abiria kubeba idadi ndogo ya abiria.

You can share this post!

Majaji Chitebwe na Muchelule wakamatwa

BENSON MATHEKA: Serikali haifai kupuuza ripoti ya Human...