CHARLES WASONGA: Ruto akabili ubadhirifu, ufisadi kufufua uchumi

CHARLES WASONGA: Ruto akabili ubadhirifu, ufisadi kufufua uchumi

NA CHARLES WASONGA

RAIS William Ruto amechukua hatua yenye busara kwa kuamuru Hazina ya Kitaifa kupunguza Sh300 bilioni kutoka kwa mgao wa fedha wa wizara za serikali mwaka huu 2022.

Akihutubu bungeni Alhamisi wiki jana, Dkt Ruto alisema kuwa hatua itaondolea serikali mzigo mzito wa kufadhili bajeti ya Sh3.2 trilioni iliyowasilishwa mwaka huu na Waziri wa Fedha anayeondoka Ukur Yatani.

Kimsingi, Rais Ruto anataka Wizara zipunguze bajeti zao za matumizi yasiyo ya kimaendeleo ili fedha nyingi zielekezwe kwa matumizi muhimu kama mipango ya kukabiliana na baa la njaa.

Kiongozi wa taifa aliwaambia wabunge waziwazi kwamba serikali inakabiliwa na changamoto za kifedha na haina budi kupunguza matumizi yake.

Kwa hivyo, inatarajiwa kwamba leo Wizara ya Fedha itawasilisha Bajeti ya Ziada Bunge la Kitaifa ili wabunge wajadili na kupitisha agizo hilo la Rais Ruto.

Ingawaje hili wazo, la kupunguza matumizi ya serikali kwa kima cha Sh300 bilioni ni bora, sidhani kama litakuwa na manufaa yoyote kwa serikali ikiwa haitaweka mipango madhubuti ya kupambana na jinamizi la ufisadi.

Pili, hatua hii haitasaidia chochote ikiwa Rais Ruto hatapambana na kero la ubadhirifu serikalini.

Tatu, kupunguzwa kwa matumizi ya serikali hakutakuwa na manufaa yoyote kwa serikali na wananchi ikiwa kwa mfano wabunge wataendelea na uchu wao wa kushikiniza Tume ya Mishahara (SRC) irejeshe baadhi ya marupurupu yao iliyoondoa Julai 2022.

Tafiti nyingi zimeonyesha kuwa ufisadi ni kikwazo kikubwa cha maendeleo nchini Kenya na hufyonza takriban Sh600 bilioni serikalini kila mwaka.

Mnamo Januari 18, 2021, mtangulizi wa Rais Ruto, Uhuru Kenyatta, alifichua kuwa serikali hupoteza Sh2 bilioni kila siku kupitia sakata za ufisadi.

Dkt Ruto, ambaye alikuwa akihudumu kama Naibu Rais wakati huo, hakupinga dai hilo kama ilivyokuwa ada yake kupinga baadhi ya kauli za bosi wake.

Kwa hivyo, endapo serikali hii ya Kenya Kwanza haitaimarisha vita dhidi ya ufisadi mipango yake ya kupunguza bajeti ya kitaifa haitakuwa na tija yoyote kwa nchi.

Kwa upande mwingine, ilikuwa kinaya kwamba Dkt Ruto alipendekeza kuwa maseneta watengewe fedha zaidi za kuendesha shughuli za ukaguzi wa utendakazi wa serikali za kaunti huku akidai serikali haina fedha.

Aidha, Rais Ruto hakujitokeza wazi na kupinga shinikizo za wabunge za kutaka marupurupu zaidi ilhali njia moja ya serikali kuokoa fedha ni kuondolewa kwa malipo kama hayo.

Data kutoka SRC inaonyesha kuwa watumishi wa umma, wabunge na maafisa wengine wa serikali hulipwa marupurupu 247 tofauti. Hii ni kando na mishahara yao.

Kwa hivyo, tasnifu yangu ni kwamba Rais Ruto aimarishe vita dhidi ya ufisadi na azime ubadhirifu serikalini ili kufikia malengo yake ya kufufua uchumi.

Katika bajeti ya kitaifa ya mwaka huu wa kifedha wa 2022/2023 serikali inalenga kukusanya Sh2.1 trilioni kama ushuru wa moja kwa moja.

Hata hivyo, inapanga kutumia jumla ya Sh2.25 trilioni kwa matumizi ya kawaida ikiwemo ulipaji mishahara.

Hii ina maana kuwa serikali inakabiliwa na upungufu wa kima cha Sh846 bilioni katika bajeti, pesa ambazo italazimika kupata kwa kukopa kutoka nje na mashirika ya kifedha ya humu nchini.

Kwa hivyo, tasnifu yangu ni kwamba Rais Ruto aimarishe vita dhidi ya ufisadi na azime ubadhirifu serikalini ili kufikia malengo yake ya kufufua uchumi.

  • Tags

You can share this post!

BENSON MATHEKA: Ni makosa maafisa kama Amoth kuhudumu kama...

SHINA LA UHAI: Ugonjwa wa tezi umeanza kuweka wadau wasiwasi

T L