CHARLES WASONGA: Serikali itumie busara kuhusu suala kuu la kilimo misituni

CHARLES WASONGA: Serikali itumie busara kuhusu suala kuu la kilimo misituni

NA CHARLES WESONGA

RAIS William Ruto pamoja na Naibu wake Rigathi Gachagua wanapojizatiti kutaka kuonekana kuwa wameanza kazi kwa kishindo wawe makini wasije wakafanya maamuzi yenye madhara mengi kwa wananchi kuliko faida.

Kwa mfano, japo uamuzi wa kurejeshwa kwa mpango wa kilimo kwenye misitu utachangia kuimarika kwa uzalishaji wa chakula nchini, mpango huo unaweza kuchangia uharibifu wa misitu.

Mpango huo, unaojulikana kimombo kama “Shamba System” ulipigwa marufuku mnamo 2004 na serikali ya Rais wa zamani Hayati Mwai Kibaki.

Waziri wa Mazingira, Mali Asili na Wanyamapori, wakati huo, Dkt Newton Kulundu, alisema mpango huo ulizimwa kwa sababu ilibainika baadhi ya watu waliutumia kama kisingizio cha kuharibiwa kwa misitu.

Chini ya “Shamba System” Shirika la Huduma kwa Misitu (KFS) liliwaruhusu watu wanaoishi karibu na misitu kukuza mazao ya chakula ndani ya misitu hiyo huku wakiitunza.

Lakini baadaye serikali iligundua kuwa watu hao hao, kwa kushirikiana na matajiri na watu wenye ushawishi serikalini, waliendesha ukataji miti haswa katika misitu ya kiasili kama vile Mau.

Lakini akihutubu katika ibada ya mazishi ya Naibu Gavana wa Baringo Charles Kipng’ok, katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Solian, Kaunti ya Baringo, Bw Gachagua alitangaza kuwa serikali ya Kenya Kwanza itarejesha mpango huo wa “Shamba System” kama sehemu ya juhudi zake za kuimarisha uzalishaji chakula.

Kwa mtazamo wangu, hilo ni wazo zuri lakini limetolewa pasina kuzingatia taratibu na kanuni hitajika. Pili, tangazo hilo lilitolewa katika muktadha usiofaa- hafla ya mazishi.

Wakati kama huu ambapo, taifa la Kenya na ulimwengu kwa ujumla linapambana na athari za mabadiliko ya tabianchi, serikali inafaa kuwa makini inapotekeleza sera zinazohusiana na changamoto hii.

Ukweli ni kwamba tatizo hili, la mabadiliko ya tabianchi, linasababishwa na uharibifu wa mazingira, haswa miti, na uchafuzi wa hewa unaosababishwa na shughuli za viwanda katika mataifa ya ulimwengu.

Kwa hivyo, suala hili la kurejeshwa kwa mpango kama huu, wa kilimo misituni, ambao unaweza kutoa mwanya kwa watu wenye nia mbaya kuharibu misitu, linapasa kujadiliwa katika baraza la mawaziri kwanza.

Sababu ni kwamba hili ni suala la kisera na maamuzi kulihusu hayafai kutolewa kiholela alivyofanya Bw Gachagua juzi.

Aidha, hata baada ya kupitishwa katika baraza la mawaziri pendekezo hilo lapaswa kuwasilishwa bungeni na kujadiliwa kwa kina.

Kwa upande wao wabunge kupitia Kamati ya Kuhusu Mazingira na Mali Asili sharti waandae vikao vya kukusanya maoni na mapendekezo kutoka kwa umma, kufungamana na hitaji la kipengele cha 118 cha Katiba ya sasa.

Huu ndio mkondo ambao Bw Gachagua anapaswa kuhakikisha kuwa umefuatwa kabla ya pendekezo lake kuanza kutekelezwa.

Naonya kwamba endapo serikali haitafuata utaratibu huu, wa kisheria na kikatiba, misitu yetu, haswa ile ya kiasili, itaharibiwa kiholela.

  • Tags

You can share this post!

Napiga chafya kupindukia, mbona?

BENSON MATHEKA: Serikali iweke mikakati ya kulinda wakulima...

T L