CHARLES WASONGA: Serikali iweke mikakati ya kuzuia mlipuko wa ‘monkeypox’

CHARLES WASONGA: Serikali iweke mikakati ya kuzuia mlipuko wa ‘monkeypox’

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI ya Kitaifa na zile za kaunti zinafaa kuweka mikakati ya mapema kuzuia mkurupuko wa ugonjwa hatari wa ‘monkeypox’ nchini.

Ugonjwa huo uliripotiwa kwa mara ya kwanza katika mataifa kadhaa ya Afrika Magharibi na sasa umeripotiwa katika mataifa ya bara Uropa na Amerika.

Natoa wito huu kwa sababu japo maambukizi ya Covid-19 yamepungua, athari zake bado zinaonekana katika sekta mbalimbali za uchumi.

‘Monkeypox’ inaathiri ngozi ya mwanadamu na dalili zake zinafanana na ugonjwa wa ndui (smallpox) ambao husambaa kupitia watu kutagusana.

Dalili zake ni kama vile, kupanda kwa joto mwilini, maumivu ya kichwa na kwenye misuli, kufura kwa mwili, uchovu na kutokea kwa upele usoni na mikono.

Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limeripoti kuwa ugonjwa huu, unaosababishwa na aina fulani ya virusi, umekuwa ukisababisha vifo katika mataifa kadhaa ya Afrika Magharibi.

Wanasayansi wanasema kuwa ugonjwa huo pia huambukizwa wanyama kama vile tumbili na panya ambao huishi karibu na makazi ya binadamu.

Kulingana na WHO, ugonjwa huu huua mtu mmoja kati ya watu 10 walioambukizwa.

Vifo hivyo vimeshuhudiwa katika mataifa ya magharibi mwa Afrika kama vile Nigeria na hutokea hasusan katika maeneo ya mashambani.

Inakadiriwa kuwa Nigeria huandikisha visa 3,000, kwa wastani, vya monkeypox kila mwaka, huswa katika vitongoji duni.

Lakini ni watu ambao hujiwasilisha katika vituo vya afya kwa ajili ya kupimwa ndio hupatina na ugonjwa huo.

Hii ina maana kuwa huenda kuna watu ambao huenda wameambukizwa lakini hawajagunduliwa.

Wiki iliyopita visa vya maambukizi ya ‘monkeypox’ viligunduliwa katika nchini za Ufaransa, Ujerumani, Ubelgiji na Australia.

Awali, maambukizi yaliripotiwa katika mataifa ya Uingereza, Uhispania, Ureno, Italia, Amerika, Uswidi na Canada, wengi wa walioathirika wakiwa wanaume wa umri wa chini ambao hawakuwa wamezuru mataifa ya Afrika.

Kwa mfano, mnamo Ijumaa wiki jana, Uingereza iliripoti visa 11 vipya kwa ugonjwa huu huku wahudumu wa afya wakiwataka wananchi kuchukua tahadhari.

Kwa sababu Kenya hupokea wageni kutoka kwa mataifa haya ambako maambukizi ya ‘monkeypox’ yameripotiwa Wizara ya Afya na asasi za afya katika ngazi za kaunti sharti ziweke mikakati ya kuzuia mlipuko wa ugonjwa huo nchini.

Sawa na ilivyo katika mataifa ya magharibi mwa Afrika ugonjwa huu unaweza kusambaa kwa kasi haswa katika maeneo ya mashambani na mitaa ya mabanda nchini Kenya.

Ingawa hamna chanjo mahsusi ya kutoa kinga dhidi ya ‘monkeypox’ wataalamu wanasema kuwa chanjo ya ‘smallpox’ ina uwezo wa kukabiliana na ugonjwa huu.

Kwa kuwa chanjo hii inaweza kupatikana, Wizara ya Afya inafaa kuanza kununua chanjo hiyo na kuzisambaza haswa katika kaunti zilizoko maeneo ya mipaka kati ya Kenya na nchi jirani.

Wageni wanaoingia nchini pia walazimishwe kuwa na cheti kinachoonyesha kuwa hawana virusi vya ‘monkeypox’, ilivyofanyika baada ya mlipuko wa Covid-19.

Maafisa wa afya watumwe katika maeneo hayo na viwanja vya kimataifa vya ndege kuwapima wasafiri kutoka ng’ambo.

Natoa tahadhari hii kwa sababu, sawa na Covid-19, ugonjwa huu mpya unasambazwa na virusi hatari na hauna tiba kamili.

Ama kwa hakika wakati huu ambapo uchumi haimarika baada ya kuporomoshwa na janga la corona, serikali inafaa kufanya kila iwezalo kuzuia mkurupuko wa ugonjwa mwingine hatari.

  • Tags

You can share this post!

DKT FLO: Uvimbe pajani, tiba ipi?

TUSIJE TUKASAHAU: Dkt Ruto asiwe wa kuwachenga wanawake,...

T L