CHARLES WASONGA: Sheria zilizoko zitumiwe kudhibiti sekta ya biashara za vyuma vikuu

CHARLES WASONGA: Sheria zilizoko zitumiwe kudhibiti sekta ya biashara za vyuma vikuu

Na CHARLES WASONGA

HATUA ya Rais Uhuru Kenyatta ya kuzima biashara ya vyuma vikuu kuu nchini italegeza kwa kiwango fulani uharifu wa miundo msingi muhimu kama vile nguzo za kusambaza umeme uliosababisha kupotea kwa stima nchini juzi.

Kiongozi wa taifa alisema marufuku hiyo itaendelea kutekelezwa hadi wakati ambapo serikali itaweka mwongozo utakaohakikisha kuwa vyuma vinavyouzwa sio vile vinavyotolewa kutoka kwa nguzo za stima, reli au barabara. Hakufichua ni lini mwongozo huo utatolewa.

Rais Kenyatta aliwaamuru maafisa wa polisi kuwakamata wafanyabiashara wa vyuma hivyo ambao watakaoidi marufuku hiyo inayolenga kuzuia uharibifu wa miundo mbinu ya serikali inayotoa huduma muhimu kwa Wakenya.

Hatua iliyochukuliwa na Rais Kenyatta, japo ni ya muda, ina umuhimu mkubwa ikizingatiwa kuwa mojawapo ya sababu zilizochangia kuanguka kwa nguzo za stima katika eneo la Imara Daima, Nairobi, ni uharibifu uliosababishwa na wezi wa vyuma.

Itachangia katika kuzima uovu huo ambao kwa muda mrefu, umesababisha uharibifu wa nguzo zinazopitisha nyaya za stima na mawasiliano pamoja na vyuma vya kudhibiti reli, barabara na madaraja.

Lakini kwa kutazama upande mwingine wa sarafu ni wazi kuwa marufuku hii itaathiri watu wengi ambao wamekuwa wakitegemea biashara ya vyuma vikuu kuu kama njia ya kujipatia riziki.

Kwanza, ni wafanyabiashara waliofungua vituo vya kununua kutoka kwa watu na kuziuzia kampuni za kuyeyusha vyuma ili kutengeneza bidhaa mbalimbali.

Vituo kama hivi sasa vitafungwa kwani wenye watahofia kukamatwa kwa kukiuka amri ya Rais. Hii ni licha kwamba biashara hizi zimesajiliwa kisheria, zikapewa leseni za kuhudumu na hulipa ushuru hitajika kwa serikali za kaunti na Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA).

Hii ina maana kuwa kufungwa kwa biashara kama hizi ni pigo kwa watu, haswa vijana, ambao huziuzia vyuma. Watu kama hawa huzunguka mitaani na vijijini wakikusanya mabaki ya vyuma ili kuuza katika vituo hivi, lakini sasa wamekosa chanzo cha mapato kufuatia marufuku iliyowekwa na Rais

Wafanyabiashara hawa hununua mabaki ya vyuma kwa bei ya wastani ya Sh60 kwa kilo jijini Nairobi na maeneo ya karibu.

Kwa kutoa marufuku hiyo, Rais Kenyatta alionekana kuashiria kuwa hamna sheria ya kudhibiti sekta ya biashara ya vyuma vikuu kuu nchini. Hii ndio maana alisema kuwa marufu hiyo itadumu hadi “serikali itakapobuni mwongozo utakaohakikisha kuwa vyuma vinavyouzwa sio vile vinavyotolewa kutoka kwa nguzo za stima, reli au barabara.”

Ukweli ni kwamba kuna Sheria ya Kudhibiti Biashara ya Vyuma Vikuu Kuu (Scrap Metal Act) ambayo Rais mwenye aliitia saini mnamo Novemba 13, 2015. Sheria hiyo inapendekeza kubuniwa Baraza la Kusimamia Biashara ya Vyuma Vikuu Kuu, kusimamia masuala yote katika sekta hiyo ambayo hutegemewa na zaidi ya watu milioni mbili nchini.

Mojawapo ya majukumu ya baraza hili ni kukagua vyuma vinayouzwa katika vituo mbalimbali nchini ili kuhakikisha kuwa sio vile vinavyoibiwa kutoka kwa nguzo za stima, reli na madaraja.

Pili, mswada wa marekebisho ya sheria ya Kawi na Mawasiliano ulipitishwa bungeni na kutiwa saini na Rais Mstaafu Mwai Kibaki mnamo Julai 2011. Sheria hiyo inaweka mikakati ya kuzuia uharibifu wa nyaya za umeme na mawasiliano.

Kwa hivyo, serikali inapaswa kutekeleza sheria hizi kikamilifu badala ya kuweka mafuruku kama inayoathiri hata wale wanaotii sheria zilizoko sasa.

  • Tags

You can share this post!

Oparanya kutetea kiwanda cha sukari

TUSIJE TUKASAHAU: Mudavadi ajue Ruto ni sehemu ya serikali...

T L