CHARLES WASONGA: Si wakati mwafaka wa kuadhimisha ya Siku ya Katiba

CHARLES WASONGA: Si wakati mwafaka wa kuadhimisha ya Siku ya Katiba

Na CHARLES WASONGA

JUZI aliyekuwa mpiganiaji wa ukombozi wa pili nchini Koigi Wamwere aliisuta Serikali Kuu kwa kutoandaa maadhimisho ya miaka 11 tangu kuzinduliwa kwa Katiba ya sasa.

Katiba hii ilizinduliwa rasmi mnamo Agosti 27, 2010 katika uwanja wa Uhuru Park, Nairobi, hafla iliyoongozwa na Rais mstaafu Mwai Kibaki.

Kulingana na Bw Wamwere, ambaye pia ni Mbunge wa zamani wa Subukia, siku hiyo inapaswa kutengwa kama siku ya kitaifa ili kutoa nafasi kwa Wakenya kutathmini manufaa na mapungufu ya Katiba hii.

Naheshimu pendekezo la mwanasiasa huyo mkongwe lakini sikubaliani nalo. Kwa mtazamo wangu maadhimisho anayoyarejelea hayatakuwa na maana yoyote wakati kama huu ambapo Katiba hii haijatekelezwa kikamilifu.

Kwa bahati mbaya wanaopinga marekebisho ya Katiba hawafanyi lolote kuhimiza utekelezaji wake kwa ukamilifu.Ukweli ni kwamba kipengele cha 43 kuhusu Haki za Kimsingi za raia, kipengele cha 81 kuhusu uwepo wa usawa wa jinsia katika afisi za umma na vipengele vyote katika Sura ya Sita vinavyohusu maadili na uongozi bora katika afisi za umma havijatekelezwa ilivyodhamiriwa.

Kwa mfano, endapo kipengele cha 43 kitatekelezwa kikamilifu, serikali ingeweza kufanikisha tatu kati ya Ajenda Nne Kuu za Maendeleo za serikali ya Jubilee na malengo mengi katika Ruwaza ya Maendeleo ya 2030.

Hii ni kwa sababu kulingana na kipengele hiki ni wajibu wa serikali kuhakikisha kuwa kila Mkenya anapata afya bora kwa gharama ya chini, elimu bora ya kimsingi, anaishi katika nyumba nzuri, anapata chakula bora na anaishi katika mazingira salama na safi.

Swali langu kwa Bw Wamwere na wengine wenye fikra kama zake ni je, kuna haja gani kwa Serikali kuandaa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Katiba ilhali haijatoa mahitaji haya kwa raia?

Raia bado wanakabiliwa na ukosefu wa chakula, huduma za matibabu kwa gharama nafuu na elimu ya msingi kwa wote, miaka 11 baada kuzinduliwa kwa Katiba hii.Juzi Serikali ilitoa ilani kwamba jumla ya kaunti 23 kati ya 47 zinakabiliwa na baa la njaa kutokana na kiangazi.

Nyingi za kaunti hizo ni zile zilizoko Kaskazini na Kaskazini Mashariki mwa Kenya na ambazo zinahitaji chakula cha msaada kwa dharura.

Kinaya ni kwamba serikali imefeli kabisa kufanikisha miradi ya kuzalisha chakula kupitia kilimo cha unyunyiziaji mashamba maji.Mfano ni mradi wa Galana Kulalu ambao umefeli kabisa kufikia lengo lake la kuzalisha zaidi ya magunia 40 ya mahindi kila mwaka.

Hii ndio mojawapo ya sababu zinazochangia Wakenya kukabiliwa na baa la njaa kila mwaka.Vile vile, endapo serikali itahakikisha Sura ya Sita ya Katiba ya sasa imetekelezwa ipasavyo, ufisadi na maovu mengine ya kimaadili katika sekta ya umma yatapunguza kwa kiwago kikubwa.

You can share this post!

Arsenal watumia Sh22.8 bilioni kujisuka upya msimu huu

MARY WANGARI: NHIF yahitaji mageuzi ili kuboresha huduma