CHARLES WASONGA: Tukatae mswada wa kulipia wabunge bima ya afya

CHARLES WASONGA: Tukatae mswada wa kulipia wabunge bima ya afya

Na CHARLES WASONGA

MWENENDO wa wabunge kujitakia makuu kila uchaguzi unapokaribia, jinsi inavyodhihirika katika mswada utakaojadiliwa bungeni wiki hii, unafaa kukataliwa kabisa.

Kulingana na mswada huo wa marekebisho ya Sheria ya Pensheni, uliodhaminiwa na Kamati ya Bunge kuhusu Utekelezaji wa Katiba (CIOC), wabunge wanamtaka mlipaushuru agharamie bima yao ya afya baada yao kuondoka bungeni.

Ikizingatiwa kuwa, kwa wastani, asilimia 75 ya wabunge hupoteza viti vyao katika chaguzi kuu; ni bayana kwamba wanasiasa wanataka kuwabebesha wananchi gharama kubwa ya matibabu yao, baada yao kubwagwa kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Bila shaka ikiwa Bunge litapitisha mswada huo na Rais Uhuru Kenyatta autie saini ili kuwa sheria, serikali haitakuwa na budi ila kuwaongezea wananchi ushuru zaidi mwaka ujao wa fedha 2022/2023.

Hii ndio maana naomba wananchi kutumia majukwaa mbalimbali kupinga pendekezo hili, sababu ni wao wataumia zaidi likipitishwa.

Rais Kenyatta naye akatae kutia saini mswada kama huo endapo utapitishwa na wabunge – dalili zote zinaonyesha kuwa wataupitisha.

Kulingana na sheria inayoongoza bima ya afya, mtu yoyote hafai kunufaika na bima hiyo pasipo kutoa mchango wake wa kila mwezi.

Ni maafisa wakuu pekee; kama Rais, Naibu Rais, Waziri Mkuu, Jaji Mkuu na Maspika wa mabunge mawili ya kitaifa (Bunge na Seneti), ambao kisheria wanaweza kuendelea kunufaika na bima ya afya inayolipwa na pesa za umma baada yao kustaafu.

Maafisa hawa hupata manufaa hayo kuambatana na Sheria ya Kustaafu kwa Naibu Rais na Maafisa Wengine Wakuu, iliyopitishwa mnamo 2015.

Hivyo, ni kitendo cha ulafi na wizi wa pesa za umma kwa wabunge kutaka walipiwe bima ya afya watakaposhindwa kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Ikiwa wabunge wanachama wa kamati ya CIOC, wakiongozwa na mwenyekiti Jeremiah Kioni, wanataka kuendelea kufurahia bima ya afya baada ya kuondoka kitini, itawabidi wailipie wao wenyewe.

Wasielekeze mzigo huo kwa Wakenya ambao tayari wanazongwa na matatizo mazito ya kupanda kwa gharama ya maisha kufuatia janga la Covid-19.

Nakumbuka kwamba mwaka jana, Rais Kenyatta aliwafaa Wakenya zaidi alipokataa kutia saini mswada wa marekebisho ya sheria ya pensheni za wabunge.

Mswada huo ulikuwa umependekeza kwamba, wabunge waliostaafu kuanzia 1984 wawe wakipokea malipo ya Sh100,000 kila mwezi.

Pendekezo hilo pia lilikataliwa na Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) ambayo ilisema kwamba haikushauriwa kama inavyoagiza kipengele cha 260 cha Katiba ya sasa.

Kwa mara nyingine, naomba Rais Kenyatta awe mkakamavu kukataa mswada huu wa bima ya afya, kwani hatua yake itakuwa kwa manufaa ya Wakenya.

You can share this post!

FAUSTINE NGILA: Tuna kibarua kukuza miji ya kibiashara na...

Akamatwa kwa kumfanyia mpenziwe mtihani