CHARLES WASONGA: Ushirikiano wahitajika kuzuia ajali msimu huu

CHARLES WASONGA: Ushirikiano wahitajika kuzuia ajali msimu huu

Na CHARLES WASONGA

MOJAWAPO ya sababu zilizochangia vifo vya zaidi ya watu 23 baada ya basi walilokuwa wakisafiria kusombwa katika mto Enziu uliofurika Mwingi ni shinikizo za abiria kwa dereva.

Kulingana na ripoti za maafisa wa polisi na shuhuda za manusura wa mkasa huo, baadhi ya wanakwaya walioabiri basi hilo lililokuwa likiwasafirisha kwenda harusini, walisisitiza dereva huyo awavukishe ili wasichelewe kufika mahala pa sherehe.

Hii ni licha ya kwamba, kulingana na ripoti hizo, dereva wa basi hilo la Shule ya Kibinafsi ya Mwingi Junior Seminary aliwaambia kuwa hakuelewa kina cha mto huo ambao husababisha maafa kila mara.Hii inaaashiria kuwa dereva huyo alikuwa mgeni katika barabara hiyo.

Wakazi wa eneo hilo pia walimuonya dereva huyo dhidi ya kuvuka mto huo uliofurika, kutokana na mvua kubwa inayonyesha eneo hilo, lakini akawapuuza na kutii abiria wake.Walisema licha ya matatu moja na trakta kuvuka salama, basi hilo halingeweza kuvuka kwa sababu lilibeba abiria wengi kupita kiasi.

Kwa mara nyingine mkasa huu ni funzo kwa Wakenya msimu huu wa sherehe ambapo wengi watakuwa wakisafiri kutoka mijini kuelekea mashambani kujumuika na jamaa zao.Wengine watakuwa wakisafiri kuelekea pwani ya Kenya na maeneo mengine ya starehe kusherehekea Siku Kuu ya Krismasi na Mwaka Mpya.

Ipo haja kwa wananchi kuwa makini zaidi na wakome kuabiri mabasi na matatu ambayo hayajazoea kutumia ruti fulani ili kuzuia mkasa sawa na ule ambao ulitokea Mwingi juzi.Kwa mfano, wakati kama huu baadhi ya matatu zinazohudumu katika ruti za Nairobi na maeneo ya karibu a huamua kubeba abiria wa kuelekea magharibi mwa Kenya au maeneo ya Mlima Kenya kutokana na ongezeko la abiria wanaosafiri mashambani.

Japo hii ni kinyume cha sheria za Bodi ya Kutoa Leseni kwa Magari ya Uchukuzi (TLB) wahudumu wa magari hayo hutoa hongo kwa maafisa wa trafiki na hivyo kukwepa adhabu. Ni rahisi kwa madereva kama hawa kusababisha ajali kwa kukosa ufahamu wa hali ya barabara za maeneo ya mashambani haswa katika msimu huo wa mvua nyingi.

Pili, ni wakati kama huu ambapo magari mengi huamua kubeba abiria wengi kupita kiasi na madereva kuendesha kwa kasi ya juu ili kuvuna faida kubwa.Wananchi ambao watakuwa wakisafiri kutoka mijini kuelekea maeneo ya mashambani kujumuika na wapendwa wao kwa sherehe mbalimbali waepuke magari kama haya.

Isitoshe, raia wakome kutumia magari ya kibinafsi ambayo hayana leseni ya kuyaruhusu kubeba abiria. Magari kama hayo ni hatari kwa usalama na maisha yao.Kulingana na takwimu zilizotolewa na Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS) Septemba 21 mwaka huu, idadi ya watu waliofariki katika ajali za barabarani iliongezeka hadi 3,975 mwaka jana kutoka 3,586 mnamo 2019.

Hii ni licha ya kwamba serikali ilikuwa ikitekeleza masharti makali ya kuzuia kuenea kwa ugonjwa hatari kama vile kafyu na marufuku ya kusafiri.kutoka kaunti moja hadi nyingine. Hii ina maana ya kwamba wakati huu ambapo masharti hayo mawili yameondolewa kutakuwa na safari nyingi zaidi katika msimu huu wa sherehe mwaka huu.

Kwa hivyo, madereva, wakuu wa mashirika ya matatu (SACCOs), maafisa wa usalama na wananchi wanafaa kushirikiana ili kupunguza ajali za barabarani.

You can share this post!

KDF wadaiwa kutesa wananchi barabarani

TAHARIRI: Ni msimu wa Krismasi kila mmoja awe mwangalifu

T L