CHARLES WASONGA: Vyuo vikuu vishirikiane na soko la ajira ili kuzalishia wahitimu kazi

CHARLES WASONGA: Vyuo vikuu vishirikiane na soko la ajira ili kuzalishia wahitimu kazi

NA CHARLES WASONGA

VYUO Vikuu ni miongoni mwa asasi kuu za mafunzo ambazo hutegemewa katika uzalishaji wa wafanyakazi ambao hutarajiwa kuendesha magurudumu ya maendeleo katika sekta zote za uchumi.

Lakini kuanzia mwaka wa 1997 hadi sasa idadi kubwa ya wanafunzi ambao hufuzu kila mwaka kutoka kwa vyuo hivi hukosa ajira katika sekta ya umma na ile ya kibinafsi.

Japo kero hili la ukosefu wa ajira kwa wahitimu kutoka vyuo vikuu huchangiwa na idadi kubwa ya wahitimu hao, shida hiyo pia huchangiwa na aina za kozi zinafunzwa katika vyuo hivi.

Utafiti umeonyesha kuwa nyingi za kozi hizo, haswa zile zinazofundishwa katika vyuo vikuu vya umma huwa havilandani na mahitaji ya soko la ajira.

Isitoshe, baadhi ya kozi hizo huwa hazijaidhinishwa na Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu (CUE) au mashirika mbalimbali ya kitaaalum.

Kwa mfano, mnamo 2017 katika ripoti yake kwa jina “Status of Higher Education, 2016″, tume hiyo iligundua jumla ya kozi 32 zilizokuwa zikifunzwa katika vyuo vikuu vya umma havikuwa vimesajiliwa rasmi.

Ripoti hiyo pia iligundua kuwa tangu miaka ya 1980s hadi 1990s nyingi za vyuo vikuu vya umma vilikuwa vikifunza kozi za sanaa badala ya zile za sayansi na teknolojia, zinazohitajika katika soko la ajira nchini.

Isitoshe, serikali ya sasa imetambua umuhimu wa sayansi, teknolojia na uvumbuzi katika ufanikishaji wa ajenda zake nne kuu za maendeleo ilizotangaza mnamo 2017.

Hii ndio maana naunga mkono ushauri wa Kamati ya Bunge kuhusu Elimu kwa tume ya CUE kwamba inashirikiane na mashirika ya kitaalamu katika kuhakikisha kuwa kozi zinazofunzwa katika vyuo vikuu nchini vinaoana na mahitaji ya soko la ajira.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Bi Florence Mutua alisema ushiriano huu ndio utazuia tatizo la wahitimu wengi kukosa ajira baada ya masomo.

Ni jambo la kuvunja moyo kwamba serikali, wazazi na familia kwa ujumla huwekeza pesa nyingi katika elimu ya wanafunzi wa vyuo vikuu kisha baadhi yao hugeuka kuwa majambazi kwa kukosa ajira. Hii ni kwa sababu baadhi yao huwa hawana ujuzi na maarifa ya kujiajiri.

  • Tags

You can share this post!

CECIL ODONGO: Jamii ya Mulembe isake msemaji mwengine baada...

Mazao yanayonawiri maeneo kame yana mchango mkubwa...

T L