CHARLES WASONGA: Wanawake waige ujasiri wa Mama Grace Onyango

CHARLES WASONGA: Wanawake waige ujasiri wa Mama Grace Onyango

NA CHARLES WASONGA

MAISHA ya mwanamke wa kwanza nchini kuwahi kuchaguliwa mbunge, marehemu Grace Akech Onyango, ni funzo kwa wanawake nchini kwamba wanapaswa kupigania nafasi za uongozi kwa ujasiri na moyo wa kujitolea.

Ni sadfa kwamba Mama Onyango alikufa Jumatano, Machi 8, 2023; siku ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake (IWD) ya mwaka huu 2023.

Hii ni siku ambayo ulimwenguni hukumbuka mchango wa wanawake katika nyanja mbalimbali za maisha na mafanikio yao katika uboreshaji wa maisha ya wanajamii. Wasichana na wanawake walio nje na ndani ya siasa sasa wana nafasi nzuri ya kujifunza mengi kutokana mafanikio ambayo marehemu Onyango aliandikisha katika ulingo wa siasa wakati huu ambao Wakenya wanaendelea kumwomboleza.

Mbali na kuwa mwanamke wa kwanza kuchaguliwa (sio kuteuliwa) kuwa Mbunge, Mama Onyango pia anashikilia rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kuchaguliwa Meya nchini Kenya.

Alishinda kiti cha Umeya wa Kisumu mnamo 1965 kabla ya kushinda ubunge wa Kisumu Mjini, katika uchaguzi mkuu wa 1969 kwa kuwabwaga wanaume saba.

Kwa hivyo, kizazi cha sasa cha wanasiasa wa kike wanaoshikilia viti mbalimbali, pamoja na wale ambao hawajafaulu kushinda viti hivi, kinafaa kutambua kuwa Mama Onyango ndiye wa kwanza kuondoa kasumba kwamba nafasi ya mwanamke ni jikoni wala sio uongozini. Akihudumu kama Mbunge hadi 1983, Mama Onyango alionyesha weledi mkubwa katika mijadala bungeni licha ya kuwa mwanamke wa kipekee miongoni mwa wabunge 158 wa kiume.

Itakumbukwa kwamba mnamo 1976, alijitokeza kama mbunge jasiri sana aliposhirikiana na aliyekuwa Mbunge wa Butere Martin Shikuku kuificha nakala halisi ya ripoti ya uchunguzi kuhusu mauaji ya aliyekuwa Mbunge wa Nyandarua Kaskazini J M Kariuki, kabla ya kuwasilishwa Ikulu.

Hii ni baada ya kudaiwa kuwa ripoti iliyowasilishwa bungeni na aliyekuwa Mbunge Kimilili, Elijah Mwangale, ilivurugwa katika Ikulu ya Rais kwa lengo la kuficha ukweli kuhusu mauaji hayo.

Ni baada ya marehemu Mama Onyango kuvuruga taasubi potovu kwamba ulingo wa siasa na uongozi ni ‘himaya’ ya wanaume pekee ambapo wanawake wengine kama vile, Phoebe Asiyo (Karachuonyo), Grace Ogot (Gem) na Agnes Ndetei (Kibwezi) walijitosa kwenye ulingo wa siasa, wakashindania viti na kufaulu kuchaguliwa kuwa wabunge.

Aidha, Bi Nyiva Mwendwa aliteuliwa na chama cha Kanu kuwa Mbunge Maalum baada ya uchaguzi mkuu wa 1992. Mnamo 1995 Rais Daniel arap Moi alimchagua kuwa waziri wa kwanza mwanamke katika historia ya taifa la Kenya.

Bi Mwendwa alihudumu kama Waziri wa Utamaduni na Huduma za Kijamii na mwaka huo huo wa 1995 aliongoza ujumbe wa Kenya katika Kongamano la Wanawake lililofanyika jijini Beijing, China.

Ni baada kongamano hilo na kushika kasi kwa mfumo wa utawala wa vyama vingi nchini Kenya ambapo wanawake wengi walijitokeza kuwania viti mbalimbali vya kisiasa. Ndiposa Gavana wa zamani wa Kitui, Bi Charity Ngilu akaandikisha historia nyingine 1997 kwa kuwa mwanamke wa kwanza nchini kuwania urais.

Ninatoa historia hii ili kuonyesha wanasiasa wa kike wa kizazi cha sasa jinsi mbegu za matunda wanayochuma wakati huu katika ulingo wa siasa zilivyopandwa na kunawirishwa na mwendazake Mama Onyango.

Sasa ni wajibu wao kuendeleza mapambano yaliyoanzishwa na Mama Onyango kwa kupigania uwakilishi wa wanawake wengi zaidi katika ngazi za uongozi.

  • Tags

You can share this post!

Maseneta wa Azimio watishia kuvuruga ajenda za serikali...

Wazee zaidi ya 100 wapata matibabu ya bure kupitia mpango...

T L