CHARLES WASONGA: Watahiniwa waliozoa gredi za chini wasife moyo, wanaweza kupata digrii

CHARLES WASONGA: Watahiniwa waliozoa gredi za chini wasife moyo, wanaweza kupata digrii

NA CHARLES WASONGA

KUTANGAZWA kwa matokeo ya Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) kuliibua hisia mseto miongoni mwa watahiniwa, jamaa zao na Wakenya kwa ujumla.

Ilikuwa ni furaha kuu kwa watahiniwa 173,345 waliopata gredi C+ kwenda juu kwani sasa watajiunga na vyuo vikuu moja kwa moja kusomea kozi za shahada ya digrii.

Watahiniwa wengine 708,071 waliopata gredi C hadi E walisalia na fikra kwamba walifeli mtihani.

Aidha, jumla ya wanafunzi 30,822 ambao walipata gredi ya E yawezekana walihisi kufeli kabisa maishani; kwamba karo ambayo wazazi walilipa haitakuwa na manufaa yoyote maishani mwao.

Ningependa kuhimiza watahiniwa hao – karibu wote wakiwa ni matineja na vijana wachanga – wasife moyo.

Bado wana nafasi ya kujiimarisha kimasomo kisha wahitimu digrii katika taaluma watakazopenda kuzamia maishani.

Alivyosema Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu, watahiniwa wote ambao hawakupata gredi ya kuingia chuo kikuu bado wako na fursa ya kujiunga na vyuo vya kadri kusomea kozi mbalimbali hususan za kiufundi.

Isitoshe, waliopata gredi za chini zaidi kama D, D- na E wanaweza kusomea kozi za kiufundi na kuhitimu kwa Stashahada ya Cheti.

Nyakati hizi Wizara ya Elimu imetoa mwanya kwa mtu yeyote kuanza kusomea kozi kiwango cha Cheti na akapanda ngazi hadi Shahada ya Digrii.

Hivyo, watahiniwa wowote wanaweza kuingia Vyuo vya Mafunzo ya Kiufundi (TVET) kokote nchini kusomea kozi chungu nzima za kiufundi zinazofunzwa humo.

Ama kwa hakika, kuna uhaba mkubwa wa mafundi stadi na mahiri wa kazi kama vile useremala, ujenzi wa nyumba, na mafundi wa stima hasa mashambani.

Hii ina maana kwamba kuna nafasi kubwa ya waliohitimu KCSE 2022 kujiunga na TVETs wakafuzu na kupata ajira au wajiajiri kwa kufungua kazi zao wenyewe.

  • Tags

You can share this post!

CECIL ODONGO: Ruto, Gachagua polepole wanaingia mtego wa...

Joto la kisiasa lapanda Tanzania Lissu akirejea

T L