CHARLES WASONGA: Wizara ya elimu iongezee zaidi muda muhula wa pili

CHARLES WASONGA: Wizara ya elimu iongezee zaidi muda muhula wa pili

NA CHARLES WASONGA

WIZARA ya Elimu inafaa kuahirisha mitihani ya kitaifa ambayo ilikuwa imeratibiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu baada ya muda wa masomo kukatizwa na shughuli za uchaguzi.

Awali, Waziri wa Elimu George Magoha, alikuwa ametangaza kuwa shule zingefunguliwa mnamo Jumatatu, Agosti 15, 2022, lakini baadaye akasongeza siku tatu mbele ufunguzi huo hadi Alhamisi wiki hii.

Kwa kuwa Profesa Magoha aliamuru shule zifungwe mnamo Jumatano, Agosti 3, 2022, shule zikifunguliwa mnamo Alhamisi, Agosti 18, 2022, wanafunzi watakuwa wamesalia nyumbani kwa muda wa siku 13.

Hii ina maana kuwa wanafunzi watakuwa wamepoteza karibu wiki mbili, muda wa masomo. Ni wazi kuwa wale ambao wataathirika zaidi ni watahiniwa wa mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE), Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) na Mtihani wa Kitaifa wa Gredi ya 6 (KPSEA).

Kwa hivyo, endapo ni kweli kwamba shule zitafunguliwa kesho kutwa, Alhamisi, Waziri Profesa Magoha anafaa kuongeza muda wa majuma mawili kwa muhula huu wa pili katika kalenda ya masomo ya mwaka huu wa 2022.

Hatua hii itatoa nafasi kwa walimu kukamilisha silabasi kwa sababu kukatizwa kwa masomo kutoa nafasi kwa uchaguzi kumeathiri kufikiwa kwa lengo hilo ndani ya muda uliowekwa.

Hii itamaanisha kuwa mitihani hiyo mitatu ya kitaifa ambayo ilikuwa imeratibiwa kufanyika kuanzia mwezi Septemba 2022 inapasa kusongezwa mbele hadi Januari 2023.

Haitakuwa bora kwa mitihani hiyo kufanyika mwezi wa Desemba mwaka huu kwa sababu mwezi huo huwa umesheheni sherehe nyingi kama vile Siku Kuu ya Krismasi na Mwaka Mpya.

Japo, uchaguzi mkuu ni shughuli muhimu kwa uthabiti na maendeleo ya taifa la Kenya, shughuli hii haipasi kuvuruga mustakabali wa watoto wetu kimasomo.

Wana wetu ndio viongozi wa kesho na maisha yao hayafai kuvurugwa na shughuli hii ya kuwachagua viongozi ambao watashikilia nyadhifa za uongozi kati ya sasa hadi 2027.

Endapo, kesho Jumatano jioni, taharuki ya kisiasa bado itakuwa imetanda nchini, itakuwa jambo la busara kwa serikali kuahirisha tarehe ya kufunguliwa kwa shule kwa mara nyingine ili kulinda usalama wa wanafunzi.

Hakuna mzazi ataruhusu mtoto wake kusafiri kuelekea shule endapo maandamano yatakuwa yatakuwa yakifanyika katika barabara za miji mikuu nchini, ilivyofanyika baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Kulingana na kalenda ya masomo ya mwaka huu, muhula wa pili ulilkuwa umeratibiwa kufikia kikomo mnamo Septemba 16 na ule wa tatu kuanza mnamo Septemba 26, baada ya wanafunzi kupumzika kwa siku 10.

Ratiba hiyo sasa haitaweza kufuatwa kwa sababu wa muda ambao wanafunzi wamepoteza wakiwa nyumbani kutoa nafasi uchaguzi mkuu ufanyike.

Kwa hivyo, ni muhimu kwa wanasiasa ambao wameshindwa katika uchaguzi mkuu kudumisha utulivu na badala yake wawasilishe kesi za kupinga matokeo hayo mahakamani.

Hamna haja kwa wao kutoa taarifa na matamshi ya kuchochea uhasama na chuki za kikabila kwa sababu uthabiti wa taifa hili ni muhimu zaidi kuzidi ndoto zao za kutwaa nyadhifa mbalimbali.

  • Tags

You can share this post!

Hakuna Rais Mteule nchini kwa sasa, asema Raila

Raila apinga matokeo ya IEBC

T L