Habari MsetoSiasa

Chebukati aanzisha mikakati ya kuleta mageuzi makuu IEBC

August 20th, 2018 2 min read

Na PATRICK LANG’AT

MWENYEKITI wa TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati ameanzisha mikakati ya kuleta mabadiliko kwenye tume hiyo baada ya Mahakama Kuu kuidhinisha makamishna watatu waliosalia kuendelea kuchapa kazi.

Mahakama Kuu ijumaa ilisema makamishna watatu waliosalia afisini, baada ya wenzao wanne kujiuzulu, wako sawa na wanaweza kuendeleza shughuli za tume.

Miongoni mwa mipango ambayo Bw Chebukati ameratibu ni kuhamisha tume hiyo kutoka Jumba la Anniversary Towers lililoko katikati mwa jiji la Nairobi na linalomilikiwa na kampuni ya Kenya-Re.

Tume hiyo hutumia zaidi ya Sh100 milioni kwa mwaka kulipa kodi.

“Mpango wa kununua jumba litakalotumiwa kama makao makuu ya IEBC litaokoa kiasi kikubwa cha fedha ambazo tume imekuwa ikitumia kulipa kodi ya nyumba, kukodisha kumbi za mikutano na kuhifadhi vifaa vya uchaguzi,” akasema Bw Chebukati.

Bw Chebukati alisema kuhamishwa kwa makao makuu ya IEBC kutoka katikati mwa jiji la Nairobi pia kutasaidia kupunguza visa vya uvurugaji wa biashara watu wanapoandamana kupinga matokeo ya uchaguzi ya uchaguzi.

Kila wakati kunapokuwa na maandamano dhidi ya IEBC, biashara katikati mwa jiji huvurugwa hivyo kuwasababishia wafanyabiashara hasara ya mamilioni.

Bw Chebukati, hata hivyo, hakufichua wakati makao ya IEBC yatahamishwa kutoka jumba la Anniversary Towers. Lakini duru zinasema mpango huo utaanza kutekelezwa kuanzia Julai 2019.

Bw Chebukati alisema uamuzi wa Mahakama Kuu ulioidhinisha makamishna watatu kuendelea kutekeleza majukumu yao umewezesha tume hiyo kuendesha chaguzi ndogo katika eneobunge la Baringo Kusini na kinyang’anyiro cha useneta katika Kaunti ya Migori.

“Tunatarajia kuwa uamuzi huo utatuliza mjadala ikiwa makamishna watatu waliosalia afisini wana mamlaka ya kusimamia uchaguzi au la,” akasema Bw Chebukati.

Kesi iliyohoji uhalali wa makamishna watatu kuendesha shughuli za tume iliwasilishwa kwenye Mahakama Kuu baada ya makamishna Connie Nkatha, Paul Kurgat na Margaret Mwachanya kujiuzulu Aprili mwaka huu. Dkt Roselyne Akombe alijiondoa kutoka tume hiyo kabla ya uchaguzi wa marudio wa urais uiofanyika Oktoba 26, mwaka jana.

Bw Chebukati amesalia na makamishna wawili; Bw Abdi Guliye na Bw Boya Molu.

Kando na kuhamisha makao yake, tume ya IEBC pia inalenga kuwachunguza maafisa wa ngazi ya juu ili kutathmini uadilifu wao.

Alisema Wakenya watatakiwa kutoa maoni na malalamishi kuhusiana na maafisa wa ngazi ya juu kwa lengo la kufichua wafisadi.

Mwenyekiti huyo wa IEBC alisema tume imeanza mchakato wa kutathmini dosari na changamoto zilizojitokeza wakati wa uchaguzi wa Agosti 8 na Oktoba 26.

Alisema kongamano la kitaifa litakalojumuisha washikadau wote litafanyika kati ya Agosti 28 na Agosti 30.