Habari

Chebukati adai Raila ameionea IEBC katika BBI

October 24th, 2020 2 min read

Na WANDERI KAMAU

MWENYEKITI wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Bw Wafula Chebukati, amemlaumu vikali kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga na viongozi wanaounga mkono ripoti ya Jopokazi la Mpango wa Maridhiano (BBI) kwa “maonevu.”

Bw Chebukati alitaja kama maonevu, pendekezo la ripoti hiyo kwamba ni IEBC pekee inayopaswa kufanyiwa mageuzi kati ya tume zote huru za kikatiba zilizopo.

Ripoti hiyo inapendekeza IEBC kubadilishwa kabisa, kwa kupata makamishna wapya kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2022, ili kuimarisha imani ya Wakenya kwenye utendakazi wake.

Ripoti hiyo pia inapendekeza majukumu ya makamishna hao yafafanuliwe kwa njia iliyo wazi, ili kuepuka hali ambapo maafisa wake wakuu wataingiliana kiutendakazi.

Lakini kwenye taarifa jana, Bw Chebukati alisema pendekezo hilo linatokana na kesi iliyowasilishwa na muungano wa NASA katika Mahakama ya Juu kuhusu matokeo ya uchaguzi wa urais 2017, ambapo mahakama ilifutilia mbali matokeo hayo na kuagiza IEBC kuandaa uchaguzi mpya.

“Sababu kuu ya pendekezo hili inatokana na uamuzi wa Mahakama ya Juu kuhusu kesi ya uchaguzi wa urais wa 2017. Hata hivyo, linapuuza maamuzi mengine ya kesi 310 za chaguzi ambazo ziliwasilishwa dhidi ya tume, ambapo tume iliibuka mshindi kwa karibu kesi hizo zote,” akasema Bw Chebukati.

Vile vile, aliongeza kuwa pendekezo hilo ni sehemu ya juhudi ambazo zimekuwa zikiendeshwa kwa muda mrefu kwa dhamira ya kuingilia utendakazi wa tume hiyo kila baada ya uchaguzi mkuu tangu 1992.

“Mwingilio huo huwa unaathiri utendakazi wa tume. Lengo kuu la juhudi hizo ni kuwachochea wananchi dhidi ya utendakazi wa tume, ili kufanikisha pendekezo la BBI kuhusu kubuniwa kwa tume mpya,” akasema Bw Chebukati.

Ripoti hiyo, kadhalika inapendekeza mageuzi makubwa katika tume hiyo, ambapo kinyume na awali, inapendekeza vyama vya kisiasa kuwateua makamishna wanne.

Makamishna hao wataajiriwa kwa mfumo wa kandarasi, ambapo watahudumu kwa muda wa miaka mitatu.

Bw Odinga amekuwa akishinikiza mageuzi ya tume hiyo, akiitaja kuwa chanzo kikuu cha matatizo ambayo yamekuwa yakishuhudiwa kwenye chaguzi kuu, hasa wizi wa kura.

Kwa sasa, tume ina makamishna watatu pekee, akiwemo Bw Chebukati, Prof Abdi Guliye na Bw Boya Molu.

Makamishna wa awali wakiongozwa na aliyekuwa Naibu Mwenyekiti Consolata Maina, Bi Margaret Mwachanya na Bw Paul Kurgat walijiuzulu nyadhifa zao mnamo 2018 wakitaja “uwepo wa uongozi ufaao” kwenye tume hiyo.

Dkt Roselyn Akombe ndiye aliyekuwa kamishna wa kwanza kujiuzulu siku chache kabla ya marudio ya uchaguzi wa urais 2017. Alirejelea kazi yake ya awali katika Umoja wa Mataifa (UN) nchini Amerika, akidai maisha yake yalikuwa hatarini.

Tume pia imekuwa ikiendesha shughuli zake bila Afisa Mkuu Mtendaji tangu Aprili 2018, baada ya Bw Chebukati kumfuta kazi Bw Ezra Chiloba, ambaye ndiye alikuwa anashikilia nafasi hiyo.