Chebukati afichua njama kali ya Cherera na wenzake

Chebukati afichua njama kali ya Cherera na wenzake

NA CHARLES WASONGA

MWENYEKITI wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati sasa amefichua kuwa makamishna wanne waliopinga matokeo ya urais aliyotangaza Jumatano walitaka kulazimisha kufanyike duru ya pili ya uchaguzi wa urais.

Bw Chebukati alisema, Jumatano Agosti 17, 2022, kwamba wanne hao wakiongozwa na Naibu wake Juliana Cherera walitaka kumlazimisha atangaze kuwa wagombeaji wawili wakuu wa urais, Dkt William Ruto na Raila Odinga walipata idadi sawa ya kura, au hamna aliyepata idadi hitajika ya kura kuweza kutangazwa mshindi.

Kulingana na Katiba, mshindi wa uchaguzi wa urais sharti apate angalau asilimia 50 na kura moja ya kura zote zilizopigwa na kuhesabiwa na angalau asilimia 25 ya kura kutoka angalau kaunti 24 kati ya 47.

Uchaguzi huo ulionyesha ushindani mkali kati ya Dkt Ruto ambaye ni Naibu Rais na Bw Odinga ambaye aliwania kwa tiketi ya chama cha muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya.

Makamishna wanne waliopinga matokeo ambayo yalitangazwa na Bw Chebukati walikuwa ni Naibu Mwenyekiti Juliana Cherera, Francis Wanderi, Justus Nyang’aya na Bi Irene Masit.

Wanne hao ambao waliwahutubia wanahabari katika mkahawa wa Serena, Nairobi dakika chache kabla ya Bw Chebukati kutangaza matokeo ya urais walisema hawangeunga mkono matokeo hayo kwa sababu “hatua ya mwisho ya kuyafikia haikuendeshwa kwa uwazi.”

Bw Chebukati alimtangaza Dkt Ruto kuwa mshindi kwa kuzoa kura 7,176,141, sawa na asilimia 50.49, dhidi ya kura 6,942, 930 (au asilimia 48.85 ) za Bw Odinga.

Lakini Jumatano, Agosti 18, 2022, Bw Chebukati kwenye taarifa kwa vyombo vya habari alipuuzilia madai ya Bi Cherera na wenzake akisema kuwa kwa mujibu wa Katiba na Sheria ya Uchaguzi, yeye kama Msimamizi wa Uchaguzi wa Urais ndiye aliye na mamlaka ya kutangaza mshindi wa uchaguzi wa urais.

Alitaja hatua ya wenzake kupinga hatua hiyo na matokeo aliyotangaza kama ambayo inahujumu mapenzi ya watu wa Kenya katika kuchagua Rais wao.

“Hii ni sawa na kuhujumu Katiba na mamlaka ya Wakenya ya kuamua rais wao kwa njia ya kidemokrasia. Kama mwenyekiti, nilikataa kukubali matakwa yao ambayo ni kinyume cha Katiba na sheria na ndipo nikatangaza matokeo ya uchaguzi wa urais,” Bw Chebukati akasema kwenye taarifa.

Bi Cherera, Bw Wanderi, Bw Nyang’aya na Bi Masit walidai kuwa Bw Chebukati alikataa kuwahusisha katika hatua ya mwisho ya kujumlisha kura kabla ya kutangaza rasmi.

Lakini Jumatano, Bw Chebukati alisisitiza kuwa kulingana na Katiba, kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi ni wajibu wa mwenyekiti wa tume pekee.

“Wajibu huu ni wa mwenyekiti na hauwezi kutekelezwa kufuatia uamuzi wa kamati ya makamishna wote,” akaeleza.

Hata hivyo, makamishna wanne waliopinga matokeo hayo walisema kuwa hatua zote za uchaguzi, kuwasilishwa kwa matokeo katika kituo cha kitaifa cha Bomas ziliendeshwa kwa njia huru na haki.

  • Tags

You can share this post!

Chebukati sasa awataka polisi kuwakamata waliovamia maafisa...

Serikali kutoa mwelekeo wa kalenda ya masomo

T L