Utaratibu wa kukagua kura wachukua muda

Utaratibu wa kukagua kura wachukua muda

NA CECIL ODONGO

KUCHELEWESHWA kutangazwa kwa matokeo ya urais kumezidi kuzua wasiwasi nchini huku Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ikilaumu maajenti wa Naibu wa Rais William Ruto na mpinzani wake mkuu Raila Odinga.

Kufikia Ijumaa jioni, ni matokeo kutoka chini ya maeneobunge 20 kati ya 290 ambayo yalikuwa yamethibitishwa na kutangazwa rasmi na mwenyekiti wa IEBC,Wafula Chebukati.

Miongoni mwa maeneobunge hayo ni Webuye Mashariki, Aldai, Ndia, Nandi Hills, Kaiti, Moiben, Ainabkoi, Yatta, Gatundu South, Gilgil, Lamu Mashariki, Kangundo, Ol Jorok, Kathiani, Baringo ya Kati, Kipkelion Mashariki na Mwingi Kaskazini.

Chini ya maafisa wa uchaguzi 50 walikuwa wamefika Bomas, hilo likimaanisha kuwa zaidi ya matokeo kutoka maeneobunge 240 bado hayakuwa yamefikishwa.

Bw Chebukati alisema kujikokota kutolewa kwa matokeo kunasababishwa na tabia ya maajenti wa Dkt Ruto na Bw Odinga kuhangaisha maafisa wa IEBC wanaojumlisha matokeo.

Alitishia kuwafurusha maajenti wa Dkt Ruto na Bw Odinga kutoka ukumbi wa Bomas iwapo wataendelea na sumbua sumbua hizo.

Vilevile, aliwataka maajenti hao washauriane naye iwapo kuna utata au suala lolote kuhusu matokeo haya badala ya kuzingira maafisa wa tume wanaojikaza usiku na mchana kuhakikisha shughuli hiyo inakamilika.

“Fuatilia mchakato huu na stakabadhi ambazo zipo lakini msigeuke wakaguzi. Nakili dosari yoyote kisha upige ripoti. Iwapo kuna tatizo lolote, basi mnifikie binafsi ili nilishughulikie,” akasema Bw Chebukati.

Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa, IEBC itaharakisha mchakato wa kuthibitisha kura hizo mradi tu maajenti hao hawasumbui wafanyakazi wa IEBC.

Katiba inaipa tume hiyo siku saba kutangaza matokeo ya Urais ambazo zinatamatika mnamo Jumanne.

“Naamrisha kuwa kila hatua ya kukagua na kuhakiki matokeo ichukue dakika 15 kwa kila afisa wa uchaguzi. Pia, tutaongeza wafanyakazi zaidi kuimarisha kasi ya kuthibitisha kura,” akaongeza.

Kamishina wa IEBC, Abdi Guliye kwenye kikao kingine, aliwachemkia maajenti wa Dkt Ruto na Bw Odinga akisema iwapo tatizo hilo litaendelea, basi wataongeza maafisa wa usalama na kuwafurusha maajenti hao.

“Tuna usalama wa kutosha, hasa katika sehemu ya ukumbi ambapo fomu zinahakikiwa. Nawaomba wote wawe na heshima kwa wafanyakazi wa IEBC,” akasema Guliye.

Afisa Mkuu Mtendaji Hussein Marjan naye alikanusha taarifa kuwa mtandao wa IEBC ulikuwa umedukuliwa na akasema wameweka usalama wa hali ya juu kiteknolojia kwenye vifaa wanavyovitumia.

“Kuna habari feki ambazo zinaenea sana kuwa mtandao wetu ulidukuliwa, hilo si kweli,” alisema.

You can share this post!

STAA WA WIKI: Malkia mpya wa mbio za mita 5,000 anayefuata...

Mung’aro aahidi kuing’arisha Kilifi kimaendeleo

T L