Chebukati aonya dhidi ya kampeni hizi za mapema

Chebukati aonya dhidi ya kampeni hizi za mapema

Na WINNIE ATIENO

TUME ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC), imeonya wanasiasa dhidi ya kampeni za mapema zinazoendelea kuzua joto la kisiasa na taharuki nchini.

Tume hiyo pia imetangaza kuwa haina fedha za kutosha kuanza maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao.

Akiongea wakati wa hafla ya kuwakaribisha makamishna wapya wa IEBC, Bi Juliana Cherera, Bw Francis Wanderi, Bi Irene Masit na Bw Justus Nyang’aya, mwenyekiti wa tume hiyo Bw Wafula Chebukati alisema ni sharti wapewe fedha za kuandaa uchaguzi mkuu kulingana na bajeti yao.

Bw Chebukati alisema uchaguzi mkuu ujao utagharimu Sh40.9 bilioni kulingana na bajeti yao.

Hata hivyo, Hazina ya Kitaifa iliwapa Sh26.5 bilioni.

“Tuna upungufu wa fedha za kuandaa uchaguzi na ni lazima tutimize bajeti yetu ili tusimamie uchaguzi mkuu kikamilifu. Tunahitaji Sh14.6 bilioni ili tutimize malengo yetu ya uchaguzi mkuu ujao,” alisisitiza.

Bw Chebukati alionya wanasiasa dhidi ya uchochezi wakati wa kampeni zao za mapema alizosema ni kinyume cha sheria.

Alisema kulingana na sheria, kampeni zinafaa kuanza miezi mitatu kabla ya uchaguzi mkuu.

Baadhi ya wanasiasa walio na azma ya kugombea urais akiwemo Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, wamekuwa wakifanya mikutano kujipigia debe.

Bw Chebukati alisema kulingana na mipango ya uchaguzi, wanasiasa wanafaa kuanza kampeni miezi mitatu kabla ya uchaguzi mkuu.

“Kampeni za mapema na joto la siasa zinaendelea kuzua taharuki, tunawasihi wanasiasa kuwa waadilifu na kuhakikisha hawachochei umma,” aliongeza.

Hata hivyo, alisema IEBC inaendelea kushirikiana na Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC), Idara ya Mahakama, Kiongozi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na idara ya polisi kukabiliana na wanasiasa wachochezi.

Alisema wameshirikiana na vyombo hivyo ili pia kuhakikisha usalama unadhibitiwa wakati wa uchaguzi mkuu.

“Tunataka vyombo hivyo kuhakikisha usalama na amani inadumishwa wakati wa uchaguzi. Tumekongamana hapa Mombasa na NCIC, Mahakama, Kiongozi wa Mashtaka na idara ya polisi kujadili namna ya kudhibiti usalama wakati wa uchaguzi,” alisema Bw Chebukati.

Wakati huo huo, Bw Chebukati alitangaza kuwa makamishna hao watashirikiana na kufanya kazi kwa pamoja ili kuendesha uchaguzi huru bila mapendeleo.

Makamishna wa awali walikuwa na mzozo na kulumbana mara kwa mara, chanzo kilichopelekea wengine kujiuzulu na hata aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC, Ezra Chiloba kusimamishwa kazi.

Hata hivyo, Bw Chebukati alisema kundi jipya la makamishna limetangaza kujitolea mhanga kushirikiana kuendesha uchaguzi wa huru.Makamishna hao wapya waliapa kutekeleza wajibu wao kwa haki.

“Nimejiunga na IEBC kuleta uwiano na tunawaahidi Wakenya mwamko mpya,” alisema kamishna Justus Nyangaya.

Bi Juliana Cherera ambaye alikuwa mfanyakazi katika Kaunti ya Mombasa alisema watashirikiana kutekeleza wajibu wao.

“Tunataka Wakenya watulie waone kazi yetu murwa,” alisema.

Bw Chebukati alisema mwezi ujao IEBC itaanza usajili wa wapiga-kura kote nchini wakitarajia wapiga-kura milioni sita wapya.

Aliwaomba Wakenya walio na umri wa miaka 18 na zaidi wajitokeze kwa shughuli hiyo.

You can share this post!

MUTUA: Tunashangilia madikteta wakipinduliwa ila ipo hofu

Corona yachangia wanafunzi 400,000 kukatiza masomo