Chebukati apuuzilia mbali madai kuwa ‘deep state’ itayumbisha uchaguzi

Chebukati apuuzilia mbali madai kuwa ‘deep state’ itayumbisha uchaguzi

Na CHARLES WASONGA

MWENYEKITI wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati, Jumatano amepuuzilia mbali wasiwasi kwamba usimamizi wa uchaguzi mkuu huenda ukaingiliwa na maafisa wenye ushawishi serikalini.

Akiongea jijini Nairobi alipokutana na Mashirika ya Kidini, Bw Chebukati alikariri kuwa uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022 utaendeshwa kisheria na kwa njia huru.

“Mradi matokeo yatatangazwa katika vituo vya kupigia kura na matokeo kutumwa kwa kituo cha kitaifa cha kujumuisha kura, matokeo ya uchaguzi huo hayatabadilishwa kwa njia yoyote,” akaeleza.

“Haijalishi kama kuna maafisa wenye ushawishi au la. Tuko na Mpango wa Kuendesha Uchaguzi (EOP) na wahudumu wenye utaalamu mkubwa. Tutaendesha uchaguzi kwa njia huru, haki, yenye uwazi na itakayoaminika. Shughuli hii haitaingiliwa kwa njia yoyote,” Bw Chebukati akaongeza.

Mwenyekiti huyu alitoa ufafanuzi huu kufuatia madai kwamba kuna maafisa wenye ushawishi mkubwa serikalini, maarufu kama ‘Deep State’ ambao haswa wana uwezo wa kuingilia uchaguzi wa urais.

Madai hayo yalitolewa Jumanne na Gavana wa Nyandarua Francis Kimemia aliyesema kuwa ‘Deep State’ huingilia, kuelekeza na kuyumbisha matokeo ya uchaguzi wa urais.

Akiongea kwenye mahojiano katika runinga ya Citizen majira ya asubuhi, Bw Kimemia ambaye alihudumu kama Mkuu wa Utumishi wa Umma na Katibu katika Baraza la Mawaziri wakati wa utawala wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki, alidai kuwa mgombeaji wa urais anayeungwa mkono na maafisa hawa ndiye huwa na nafasi bora ya kutangazwa mshindi.

“Ukiwa na wagombeaji wawili wenye ushawishi wa kiwango cha 50- 50 na mmoja aungwe mkono na maafisa hawa wenye ushawishi mkubwa serikalini, kuna uwezekano mkubwa kwamba yule atakayeungwa mkono na kundi hili ataibuka mshindi. Mgombeaji sharti awe ni mtu mwadilifu na ambaye atakubalika na wote,” Bw Kimemia akasema.

“Lakini itakuwa muhimu zaidi ikiwa ataungwa mkono na ‘Deep State’,” akasisitiza.

Hata hivyo, Bw Chebukati alitaja changamoto za mitandao ya mawasiliano, fedha, hatua ya bunge kutopitisha sheria kama ambazo zitahujumu maandalizi yao ya uchaguzi.

You can share this post!

ODM haitambui PAA, asema Mbunge

Messi kusalia nje ya kikosi cha PSG kitakachomenyana na...