Habari MsetoSiasa

Chebukati na Chiloba kuhojiwa na bunge kwa siku nne kuhusu matumizi ovyo ya mabilioni ya pesa

March 19th, 2018 2 min read

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati akiwa na na Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo Ezra Chiloba. Picha/Maktaba

Na DAVID MWERE

MWENYEKITI wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati na Afisa Mkuu Mtendaji Ezra Chiloba, watahojiwa na bunge kwa siku nne kuhusiana na mabilioni ya pesa ambazo tume ililipa kinyume cha sheria zikiwemo Sh1.1 bilioni zilizolipwa mawakili.

Wawili hao watatakiwa kueleza kwa nini tume ililipa kampuni moja Sh50.5 milioni kwa kusafirisha karatasi za kura kwenye uchaguzi mkuu wa 2013.

Kulingana na ripoti ya mhasibu mkuu wa serikali, pesa hizo zililipwa kinyume cha sheria.

Ripoti hiyo inaonyesha kampuni hiyo haikuwa imepatiwa kandarasi na kwamba ilisajiliwa baada ya uchaguzi huo na baada ya kandarasi kutolewa.

Bw Chebukati na Bw Chiloba pia wanatarajiwa kueleza kamati ya uhasibu ya bunge (PAC) ni kwa nini IEBC ililipa kampuni za mawakili ambazo hazikuwa zimeidhinishwa kutoa huduma za kisheria kwa tume.

Ripoti ilifichua kwamba kampuni hizo zilipatiwa kandarasi moja kwa moja kinyume cha sheria. Kulingana na ripoti ya mwaka wa fedha 2015/16, mawakili 68 waliowakilisha tume walilipwa Sh2.1 bilioni ikiwa na sehemu ya madeni yaliyolimbikizwa tangu Juni 30, 2013.

Hii ni licha ya tume kueleza kuwa ni Sh1 bilioni zilizotakiwa kulipwa mawakili kama malimbikizi ya malipo yao tangu Juni 30, 2013.

Malimbikizi hayo yaligawanywa kama Sh568.6 milioni za kesi ya kupinga matokeo ya kura ya urais na Sh486.3 milioni za kesi zingine za uchaguzi.

Ripoti inasema kwamba malipo ya huduma za kisheria yalikuwa kinyume na sheria ya ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Katiba.

“Tume haikutoa stakabadhi kama ushahidi kuonyesha kesi ambazo mawakili waliiwakilisha na malipo kuthibitisha kwa nini ililipa pesa zaidi,” inasema ripoti ya Mhasibu Mkuu Edward Ouko.

Alipokuwa akikaguliwa na bunge majuzi, wakili mkuu wa serikali Kennedy Ogeto alilalamika kuwa serikali inapoteza pesa kwa sababu wizara, idara na mashirika kukosa kutafuta ushauri wa mwanasheria mkuu kabla ya kutia sahihi kandarasi.

Kwenye ripoti yake, Bw Ouko aligundua kuwa barua za kuwaagiza mawakili hao kuwakilisha tume zilitiwa sahihi na mkurugenzi wa masuala ya kisheria na sio kwa niaba ya tume..

Kamati inayosimamiwa na mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi, pia itachunguza kwa nini tume ililipa kampuni 30 za mawakili Sh328.3 milioni bila kandarasi na Sh17.8 milioni kwa kampuni ambazo hazikuwa zimeidhinishwa na zilipewa kandarasi moja kwa moja.

Bw Ouko pia anataka tume kueleza kwa nini ilibadilisha na kutumia Sh1.6 bilioni kununua, kusafirishwa, kutoa mafunzo, kufanyia majaribio na kuzinduliwa kwa vifaa vya kiektroniki vya kutambua wapigakura (EVIDs) kwenye uchaguzi mkuu wa 2013.

Aidha, imeibuka kuwa idadi ya magari yaliyosemekana yalikodiwa kusafirisha vifaa vya kura ilikuwa ya chini kuliko yaliyolipwa.