Habari

Chebukati roho mkononi

March 12th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

UAMUZI ambao Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi atautoa leo Jumanne alasiri utatoa mwelekeo kuhusu hatima ya makamishna watatu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ambao wanalaumiwa kwa kupotea kwa Sh9 bilioni wakati wa uchaguzi mkuu wa 2017.

Uamuzi huo utabaini ikiwa Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu wa Pesa za Umma (PAC) ilizingatia sheria ilipopendekeza kuondolewa afisini kwa mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati na na vilevile makamishna Boya Molu na Abdi Guliye kwa kosa la kuchangia kupotea kwa pesa hizo kupitia ukiukaji wa sheria za uagizaji bidhaa na huduma.

Kwenye ripoti yake iliyowasilishwa bungeni wiki moja iliyopita kuhusu maswali yaliyoibuliwa na Mkaguzi Mkuu wa Matumizi ya Pesa za Umma Edward Ouko, PAC inataka Chebukati na wenzake waondoke ili kutoa nafasi kwa mageuzi kamili kufanyiwa tume hiyo.

Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati. Picha/ Maktaba

Hata hivyo, ni sharti kwanza pendekezo hilo liidhinishwe na kikao cha bunge lote, suala ambalo Bw Muturi atalishughulikia katika uamuzi wake Jumanne.

“Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati na makamishna wenzake Boya Molu na Abdi Guliye wanafaa kuondoka afisini mara moja baada ya bunge kupitisha ripoti hii,” akasema mwenyekiti wa PAC Opiyo Wandayi alipowasilisha ripoti hiyo bungeni Jumanne wiki jana.

Ripoti hiyo pia inapendekeza kwamba makamishna hao wachunguzwe hii ikiwa ni baada ya kupotea kwa pesa hizo wakati wa uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017, na marudio ya uchaguzi wa urais Oktoba 26, 2017.

“Na wale watakaopatikana na hatia baada ya uchanguzi huo wachukuliwe hatua za kisheria,” ripoti hiyo ikaamuru.

Ripoti hiyo pia inapendekeza kuwa makamishna wa zamani wa IEBC Consolata Nkatha (Naibu Mwenyekiti), Margaret Mwachanya na Dkt Paul Kurgat wachunguzwa kwa tuhuma za kuingilia shughuli za utoaji kandarasi ya ununuzi wa bidha  na huduma, ikiwemo ununuzi wa Mitambo ya Kieletroniki ya kuendeshea uchaguzi (KIEMs kits) iliyogharimu Sh6.8 bilioni.

Chiloba

Kando na hayo Bw Wandayi na wenzake wanataka aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo Ezra Chiloba achukunguzwe kwa sakta hiyo na akipatikana na hatia afunguliwe mashtaka

Hata hivyo, ripoti hiyo iliporatibiwa kujadiliwa bungeni Jumatano wiki jana kiongozi wa wengi Aden Duale alipinga mapendekezo hayo, akisema zinakwenda kinyume cha Katiba.

Hatua hiyo ndiyo ilipelekea Bw Muturi kusitisha shughuli hiyo na kuahidi kutoa mwelekeo baada ya juma moja.

“Mapendekezo ya kamati hii yatakiuka katiba ikiwa yatapitishwa. Vile vile, yataleta matokeo mabaya kwa sababu hakutakuwa na tume ambayo inaweza kusimamia chaguzi ndogo endapo zitatokea. Isitoshe, kupitishwa kwa ripoti hii ya PAC kutaathiri chaguzi ndogo katika maeneo bunge ya Ugenya, Embakasi Kusini na Wajir Magharibi ambayo tayari zimetangazwa,” akasema Bw Duale ambaye pia ni Mbunge wa Garissa Mjini.

Kulingana na Mbunge huyo kuondolewa kwa makamishna wa IEBC kunafaa kufuata mwongozo uliowekwa katika kipengee cha 251 cha Katiba. Kipengee hicho pia kimetoa sababu ambazo zinaweza kusababisha hatua hiyo kuchukuliwa  dhidi ya wanachama wa tume za kikatiba na afisi huru.

Baadhi ya sababu hizo ni ukiukaji wa katiba, mienendo mibaya, kulemaa kiakili, kushindwa kutekeleza majukumu ya afisi na endapo wanachama watatangazwa kuwa wamefilisika.

Hata hivyo, Bw Wandayi na wabunge Otiende Amollo (Rarieda) na Junet Mohamed (Suna Mashariki) wanatofautiana na Bw Duale wakisema, mapendekezo ya PAC hayalengi kuwaondoa afisi makamishna hao bali inalenga kuanzisha mchakato wa kuwaondoa “kwa mujibu wa hitaji la Katiba”.

“Kamati hii inafahami hitaji la kipengee cha 251 cha Katiba. Kwa hivyo, ripoti yake sio ombi la kutaka makamishna hao waondolewe afisini. Kwa hivyo, pingamizi la Duale halina maana na linapoteza muda wa bunge,” akasema Wandayi.

Dkt Amollo alisema ikiwa bunge halitaidhinisha mapendekezo ya Kamati hiyo, itakuwa ni sawa na kuhujumu wajibu wake wa kikatiba kuhusu suala lenye umuhimu mkubwa kwa Wakenya.