Chebukati sasa akataa ‘kupangwa’

Chebukati sasa akataa ‘kupangwa’

Na WANDERI KAMAU

HATUA ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuepuka lawama za mapendeleo katika uchaguzi mkuu ujao kwa kujiondoa kwenye jopo maalum linalosimamia matayarisho ya Uchaguzi Mkuu wa 2022 imemtia mwenyekiti wake kwenye moto.

Wadadisi wanasema tume hiyo ilichukua hatua hiyo ili kuepuka lawama zilizoikumba hapo awali kuhusu usimamizi wa uchaguzi.

Hata hivyo chama cha ODM kimemkashifu mwenyekiti wa IEBC, Bw Wafula Chebukati kikisema ametiwa hofu na chama cha United Democratic Alliance (UDA) cha Naibu Rais William Ruto.

Kwenye barua aliyomwandikia Katibu wa Wizara ya Usalama, Karanja Kibicho mnamo Jumatatu, mwenyekiti wa tume hiyo, Bw Wafula Chebukati alisema waliamua kuchukua hatua hiyo ili kulinda uhuru wa IEBC “baada ya kushauriana”.

“Baada ya kushauriana na kurejelea taratibu za utendakazi za tume hii, tumeamua kujiondoa kwa njia ya hekima kwenye jopo hilo kuanzia sasa. IEBC ni tume huru, inayopaswa kuendesha shughuli zake kwa nia huru, bila kuingiliwa ama kushawishiwa kwa namna yoyote ile,” akasema Bw Chebukati kwenye barua hiyo.

Lakini kulingana na Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna, Bw Chebukati “alishawishiwa na UDA”.

“Fanya kazi yako kulingana na sheria na usitishwe na UDA iliyo na mbunge mmoja tu,” Bw Sifuna alisema.

Wengi walishangaa kwa nini Chebukati alichukua hatua hiyo ilhali alishiriki kamati hiyo kabla ya uchaguzi mkuu wa 2016.

Jopo hilo, ambalo lilibuniwa Novemba, linaishirikisha Idara ya Mahakama, Wizara ya Usalama wa Ndani, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT) na Afisi ya Mwanasheria Mkuu.

Kwenye uzinduzi wake, Jaji Mkuu, Martha Koome alisema lengo lake kuu litakuwa kubuni ushirikiano ufaao kati ya idara muhimu za serikali ili kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa katika mazingira yafaayo.

Hata hivyo, wadadisi wanasema kuna uwezekano IEBC imejiondoa katika jopo hilo ili kutoonekana kuegemea upande wowote wa kisiasa.

Katika siku za hivi karibuni chama cha UDA, ambacho kinahusishwa na Naibu Rais kimekuwa kikilalamikia hatua ya mawaziri Dkt Fred Matiang’i (Usalama wa Ndani) na Joe Mucheru (ICT) kujumuishwa kwenye jopo hilo, ilhali wamekuwa wakijihusisha kwenye siasa.

Katika barua aliyomwandikia Bw Chebukati majuzi, Katibu Mkuu wa UDA, Bi Veronicah Maina, alilalamikia hatua ya mawaziri hao kutangaza wazi watamuunga Bw Raila, katika azma yake ya kuwania urais 2022.

Aliwataka kujiondoa kwenye jopo hilo kwani huenda wakatumia ushawishi wao kuingilia uchaguzi huo.

Licha ya lawama hizo, mawaziri hao wameshikilia kuwa wataendelea kujihusisha na siasa, wakisema ni haki yao kikatiba.

“Hakuna yeyote atakayetuzuia kuendeleza majukumu yetu tutakavyo. Tuna haki kama kila Mkenya kutangaza misimamo yetu kisiasa,” akasema Dkt Matiang’i majuzi.

Hata hivyo, wadadisi wanasema hatua ya Bw Chebukati inatokana na matukio ya 2017, ambapo mrengo wa NASA uliilaumu kwa kukipendelea Chama cha Jubilee (JP).

“Lengo kuu la Bw Chebukati ni kujiepushia lawama za miaka ya hapo nyuma, ambapo tume za uchaguzi zimekuwa zikilaumiwa kwa kuvipendelea vyama vilivyo mamlakani,” asema Bw Javas Bigambo, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Kulingana naye, Bw Chebukati anataka kujenga imani ya tume hiyo miongoni mwa Wakenya na jamii ya kimataifa, ikizingatiwa uchaguzi huo unaonekana kuwa wenye ushindani mkubwa.

“Taswira ya uchaguzi wa 2022 inaonekana kuwa tofauti. Ni uchaguzi unaoonekana kuwa na ushindani mkali kati ya Bw Odinga na Dkt Ruto. Bw Chebukati anafanya kila awezalo kuepuka matukio ya 2017, ambapo Bw Odinga alikataa kushiriki kwenye duru ya pili ya uchaguzi,” akasema mchanganuzi huyo.

You can share this post!

Kipchoge, Chepng’etich roho mkononi tuzo ya...

Wakili wa Serikali aagiza Miguna aruhusiwe kurudi

T L