Chebukati sasa awataka polisi kuwakamata waliovamia maafisa wa IEBC Bomas

Chebukati sasa awataka polisi kuwakamata waliovamia maafisa wa IEBC Bomas

NA CHARLES WASONGA

MWENYEKITI wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati amewataka maafisa wa polisi kuwakamata watu waliowashambulia makamishna na maafisa wa tume hiyo katika ukumbi wa Bomas Jumatatu.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jumatano, Bw Chebukati alisema kuwa makamishna Abdi Guliye na Boya Molu na Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC Marjan Hussein Marjan walipigwa na kujeruhiwa na watu waliokuwa wameandamana na wanasiasa wakati wa shughuli ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais Agosti 15.

Bw Chebukati alitaka polisi na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kuwakamata washukiwa hao ili waathiriwa wapate haki.

“Tunahimiza kukamatwa kwa washambuliaji hawa bila kujali miegemeo yao ya kisiasa,” akasema.

Mwenyekiti huyo wa IEBC vile vile alilalamikia kile alichokitaja kama vitisho vinavyoelekezwa dhidi ya maafisa wa tume hiyo wakiwa kazini.

Bw Chebukati alisema kutokana na vitisho hivyo, baadhi ya wafanyakazi wa IEBC wamefeli kuripoti kazini wakihofia maisha yao.

“Tume hii inalalamika kuwa wafanyakazi wake ambao walifanya kazi yao kwa kujitolea katika Kituo cha Kitaifa cha kujumlisha kura za urais sasa wanatishwa, kudhulumiwa na hata kukamatwa kiholela. Hali hii inaathiri uhuru wao wa kufanya kazi,” akaongeza.

Mnamo Jumatatu vurugu zilitokea katika ukumbi wa Bomas baada ya wanasiasa wanaoegemea mrengo wa Azimio la Umoja-One Kenya kupinga kile walichodai ni hatua ya Bw Chebukati kupanga kumnyima mgombea wa urais wa muungano huo Raila Odinga, ushindi.

Bw Chebukati alidai wakati wa purukushani hizo, Profesa Guliye, Bw Molu na Bw Marjan walishambuliwa na kujeruhiwa.

Alisema hatua hiyo lilikuwa sawa na kuingiliwa kwa uhuru wa IEBC katika kusimamia, kuendesha na kutangaza matokeo ya uchaguzi wa urais.

“Tume hii itaendelea kulinda uhuru wake licha ya vitisho kutoka kwa wanasiasa na watu wengine wanaolenga kuhujumu utendakazi wake na kuizuia kuendesha uchaguzi kwa njia huru na haki,” Bw Chebukati akasema kabla ya kumtangaza Naibu Rais William Ruto kama mshindi wa uchaguzi wa urais na hivyo Rais-Mteule wa Kenya.

 

  • Tags

You can share this post!

Ruto asema mawaziri katika serikali yake watawajibishwa...

Chebukati afichua njama kali ya Cherera na wenzake

T L