Makala

Cheche za maneno kati ya viongozi Murang’a zachacha Seneta Nyutu akikaa ngumu

April 14th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

BAADHI ya viongozi Kaunti ya Murang’a katika siku za hivi majuzi wamekuwa wakirushiana cheche za maneno wenyewe kwa wenyewe kwenye mitandao ya kijamii, mmoja akiita mwingine jina zito.

Matusi hayo yanatandazwa katika mitandao mitatu, mmoja ukiwa wa mwanasiasa binafsi, mwingine ukiwa ni wa wadau wa kisiasa wa kaunti huku mwingine ukiwa ni wa viongozi wa Kaunti.

Wana mtandao kufahamasishana yanayojiri unaoitwa 021 Leaders X Communication na ambao waratibu ni mbunge wa Kigumo, Bw Joseph Munyoro na mbunge mwakilishi Bi Betty Maina.

Kando na wabunge wote wa Murang’a ambao ni saba, mtandao huo una Seneta Joe Nyutu, Gavana Irungu Kang’ata na wengine ambao ni mawaziri, makatibu na pia wasimamizi wa mashirika ya umma.

Hali imekuwa tete zaidi kiasi kwamba Waziri wa Ardhi Bi Alice Wahome hivi majuzi alijiondoa kutoka mtandao huo alipotukanwa akiambiwa kwamba yeye hujibeba kama fundi wa maji vijijini badala ya kuwa Waziri wa Maji.

Wakati akitukanwa hivyo, alikuwa Waziri wa Wizara ya Maji.

Mwingine wa hivi majuzi kujiondoa kwa mtandao huo ni mbunge wa Maragua Bi Mary wa Maua ambaye aliwekwa chini ya shinikizo kwa matusi motomoto, mengine yakilenga familia yake.

Aprili 11, 2024 katika hafla ya kutuza walemavu misaada ya kuanzisha biashara na pia kuwapa vijigari spesheli vya kusafiria chini ya uthamini wa Wakfu wa Seneta Joe Nyutu, Bi Wa Maua aliteta kwamba “kuna wetu ambao wamejaaliwa matusi lakini tunafaa kuungana pamoja tushikiliane kwa manufaa ya watu wa Murang’a”.

Wanaharakati wa kisiasa ambao wengi walikuwa wanawake na ambao walikuwa wamefadhiliwa kufika katika hafla hiyo iliyokuwa ikiandaliwa mjini Maragua waliiteka nyara kwa muda wakiimba nyimbo za kuhimiza wanasiasa kuungana pamoja badala ya kukwamilia matusi.

Bi Maina alipopewa nafasi kuhutubu, aliwasuta wanasiasa ambao “huongea kwa mdomo lakini matendo yao hayawiani na matamshi yao”.

Katika kisa cha hivi karibuni, Seneta maalum Bi Veronica Maina ambaye alikuwa amejiondoa kutoka kwa mtandao huo alirejeshwa na Bw Munyoro huku jitihada za kuwaunganisha zikishika kasi.

“Shida yetu iko tu kwa mwanasiasa mmoja ambaye hatufahamu kama ni shida ya akili aliyo nayo. Mimi binafsi nimeuliza madaktari wa kiakili na wakanifahamisha kwamba mwanasiasa huyo anaweza kuwa na ugonjwa unaofahamika kama Intermittent Explosive Disorder (IED) ambao hujiangazia kupitia hasira, matusi na fujo,” akasema mmoja wa viongozi wa kaunti hiyo.

Alisema kwamba kila mara inabidi viongozi wenzake wakae chonjo wakifuatilia ni zamu ya nani kutukanwa na mwanasiasa huyo.

Katika mtandao mwingine, mwanasiasa mmoja ameonekana akiwaelekeza wafuasi wake “muwe mkiwaita mbwa wote ambao watatuingilia”.

Kaunti hiyo huwa na mirengo minne ya kisiasa—unaomfuata Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, ulio na utiifu kwa Mbunge wa Kiharu Bw Ndindi Nyoro, wengine walio na hofu ya kuwa ndani ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) wakihofia mchujo wa 2027 na wengine ambao kwa msingi wa tahadhari huwa hawana msimamo.

Mbunge maalum, Bi Sabina Chege akiwania kuwa kiongozi wa chama cha Jubilee anaonekana kuwa kimbilio la wale wanaokwepa siasa za UDA.

Shida kuu imeonekana kukukumba walio na utiifu kwa Bw Gachagua ambao wanashindania ni nani atakuwa akipokezwa manufaa kwa niaba ya watu wa Murang’a.

Seneta Nyutu ndiye kinara wa vuguvugu la walio na utiifu kwa Bw Nyoro na hajaepuka kutusiwa na kuhujumiwa.

“Mimi utiifu wangu ni kwa Rais William Ruto na umoja wa Mlima Kenya… Kwa sasa hatuongei kuhusu siasa hizo lakini msimamo wangu unajulikana waziwazi. Nitukanwe, nifanyiwe nini… Hapo sing’atuki,” akasema.

[email protected]