Michezo

Chelsea bado inamezea mate kinda matata Vinicius Junior

August 13th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

KLABU ya Chelsea haijakata tamaa kutafuta huduma za kinda matata wa Real Madrid Vinicius Junior ambaye mapatano katika kandarasi yake yanamruhusu kuondoka tu kwa Sh89.3 bilioni.

Ombi la Chelsea la kwanza lilikataliwa Novemba 2019.

Mbrazil huyo mwenye umri wa miaka 20 amekoseshwa raha na kocha Zinedine Zidane kumchezesha kwa uchache uwanjani Santiago Bernabeu.

Chelsea iko sokoni kutafuta mshambuliaji kwa sababu Pedro,33, na Willian,32, wataondoka uwanjani Stamford Bridge baada ya kandarasi zao kukatika siku chache zilizopita.

Kiungo mshambuliaji wa Bayer Leverkusen Kai Havertz yuko juu ya orodha ya wachezaji Chelsea inatafuta.

Hata hivyo, gazeti la AS nchini Uhispania linadai kuwa Lampard pia yuko makini kusaini Vinicius anayesalia na miaka mitano katika kandarasi yake baada ya kujiunga na Real mwaka 2018 kutoka Flamengo.

Tetesi zinasema pia kuwa Vinicius anamezewa mate na Arsenal na Paris Saint-Germain.

Kinda huyo amechezea Real mechi 69 na kuona lango mara nane pekee.