Michezo

Chelsea kuchomoa silaha zote mpya dhidi ya Brighton katika EPL

September 13th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

CHELSEA watashuka kesho Jumatatu ugani American Express kuvaana na Brighton katika mchuano wa EPL utakaomshuhudia kocha Frank Lampard akitegemea zaidi silaha mpya alizojinasia muhula huu.

Chini ya ukufunzi wa mwanasoka huyo wao wa zamani, Chelsea wametumia zaidi ya Sh35 bilioni hadi kufikia sasa msimu huu ili kusajili wachezaji wapya ambao wanatazamiwa kutikisa uthabiti wa Liverpool na Manchester City katika soka ya Uingereza.

Hata hivyo, Brighton huenda wasiwe mteremko kwa Chelsea hasa ikizingatiwa jinsi walivyojisuka chini ya mkufunzi Graham Potter aliyewaongoza kusajili sare ya 1-1 katika mechi za mikondo miwili ya EPL dhidi ya Chelsea msimu jana.

Baada ya Brighton kuagana na Aaron Mooy aliyeyoyomea China kuchezea Shanghai SIPG, kocha Potter alimsajili Ben White kutoka Leeds Leeds United na kumshawishi Lewis Dunk kusaini mkataba mpya wa miaka mitano.

Idadi kubwa ya wachezaji ambao Chelsea wamesajili kufikia sasa inadhihirisha kiu ya Lampard kunyanyulia ‘The Blues’ mataji ya haiba chini ya kipindi kifupi iwezekanavyo.

Kufikia sasa, Chelsea wamesajili wanasoka sita wapya wakiwemo Thiago Silva (PSG), Malng Sarr (Nice), Ben Chilwell (Leicester City), Hakim Ziyech (Ajax), Timo Werner (RB Leipzig) na Kai Havertz (Bayer Leverkusen).

Katika msimu wake wa kwanza kambini mwa Chelsea, Lampard alitegemea sana huduma za chipukizi. Hata hivyo, aliwaongoza waajiri wake kumaliza kampeni za EPL katika nafasi ya nne, kutinga hatua ya 16-bora ya UEFA na kufika fainali ya Kombe la FA mnamo 2019-20.

Hata hivyo, Chelsea wametakiwa na kocha Lampard kuimarisha zaidi safu yao ya ulinzi kwa kusajili beki mwingine mahiri zaidi ili kuepuka masaibu ya msimu huu wa ulioshuhudia wanafainali hao wa Kombe la FA wakifunga jumla ya mabao 54 kwenye EPL.

Hiyo ilikuwa idadi kubwa zaidi ya mabao kati ya vikosi vyote vilivyokamilisha kampeni za EPL ndani ya mduara wa 10-bora kufungwa mnamo 2019-20.

“Chelsea kwa sasa ina mseto wa chipukizi na wanasoka wazoefu wenye tajriba pevu. Hiyo itakuwa sifa itakayowafanya kuwa kivutio zaidi miongoni mwa mashabiki wa EPL,” akasema Lampard katika mahojiano yake na Sky Sports.

Katika siku ya kwanza ya kampeni za EPL msimu huu wa 2020-21, Arsenal waliwatandika Fulham 3-0, Liverpool wakatolewa jasho na Leeds United kabla ya hatimaye kuwapiga limbukeni hao 4-3 ugani Anfield nao Crystal Palace wakawapokeza Southampton kichapo cha 1-0 uwanjani Selhurst Park.

Newcastle United waliwapiga West Ham United ya kocha David Moyes 2-0 katika London Stadium.