Michezo

Chelsea kufaa wanaoikabili coronavirus

March 19th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

MMILIKI wa klabu ya Chelsea Roman Abramovich amesema Millenium Hotel iliyoko Stamford Bridge itawapokea na kuwapa malazi maafisa wa afya wa serikali wanaopambana na maradhi ya Covid-19.

Klabu hiyo ilitoa taarifa hiyo jana ikisema kwamba bwanyenye huyo atagharamia kwa kipindi cha miezi mitatu, lakini ataendelea iwapo maafisa hao wataendelea na shughuli hizo hata baada ya muda huo kumalizika.

“Nina hakika baadhi ya maafisa hawa watakuwa wakifanya kazi hadi usiku na watakuwa na matatizo ya usafiri. Hivyo tumeamua kuwa makazi kama mojawapo wa mpango wetu wa kujitolea katika vita vya kupambana na ugonjwa huu hatari,” alisema.

“Makao yatatolewa kwa wale wanaofanya kazi katika hospitali za jiji hili, pamoja na wengine katika hospitali za wilaya jirani,” taarifa hiyo ilisema.

“Vyumba vitatolewa kulingana na idadi ya maafisa watakaotarajiwa plae Millennium Hotel,” iliongeza taarifa hiyo.

Millennium Hotel and Resort ambao ndio wasimam izi wa hoteli hiyo watasaidiana katika na wafanyakazi wa klabu kutoa huduma kwa maafisa hao wa afya.

Chelsea ni miongoni mwa timu zilizokumbwa na janga hilo la Covid-19, kisa cha kwanza kikihusu winga Callum Hudson-Odoi ambaye alipatikana na virusi kabla ya wachezaji wengine kuvamiwa na maradhi hayo.

Kwa sasa, wachezaji wa klabu hiyo wamejitenga kimazoezi huku uwanja wao wa mazoezo wa Cabham ukisabakia bila shughuli. Sasa imeripotiwa kwamba Odoi amepata nafuu baada ya kusumbuliwa na virusi vya corona.

Kupitia kwa mtandao wa klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Muiingereza huyo alithibitisha kwamba sasa amepona kabisa baada ya kutibiwa.

Chelsea ilikuwa imetangaza kuwa winga huyo wake alikuwa na dalili za corona na alipopimwa alibainika kuwa na virusi vya ugonjwa huo, jambo lililosababisha wafanyakazi na wachezaji wa klabu hiyo kujitenga na mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 19.

Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu akumbwe na maradhi hayo, Odoi alisema kwamba baada ya kutengwa kwa siku kadhaa kutokana na virusi hivyo sasa hivi amepona kabisa.

Hata hivyo, licha ya kupona, mwanasoka huyo amedai kwamba ataendelea na taratibu zilizopo na kuendelea kujitenga kibinafsi kwa wiki nzima.

Alisema hayo akieleza hamu yake ya kukutana na jamaa na marafiki zake baada ya muda huo kupita, pamoja na kurudi uwanjani.