Michezo

Chelsea kusukwa upya ikionana na Manchester United

October 30th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

MASHABIKI wa Chelsea wanamtarajia kocha Frank Lampard kufanya mabadiliko kadhaa vijana wake watakapovaana na Manchester United, kutafuta nafasi ya kutinga robo-fainali kwa mara ya tatu mfululizo.

Kiungo mshambuliaji Ross Barkley ambaye hakucheza mwishoni mwa wiki dhidi ya Burnley, huenda akarejea kikosini baada ya kupata nafuu.

Kiungo mchezeshaji, Pulisic ambaye alingara zaidi Jumapili katika mechi hiyo ambayo Chelsea walishinda kwa 4-2, anatarajiwa kuanza leo usiku.

Chelsea ambao msimu huu wanalenga mataji manne, wanatarajiwa kulipiza kisasi katika mechi yao ya utangulizi ya EPL.

Lakini huenda wasiwe na kiungo mahiri N’Golo Kante, Andreas Christensen na Ruben Loftus-Cheek ambao ni majeruhi.

Kwa upande wa Manchester, Paul Pogba ataendelea kukaa nje hadi Disemba, vilevile kikosi hicho cha kocha Ole Gunnar kitaingia uwanjani bila Luke Shaw, Nemanja Matic na Axel Tuenzebe. Wengine watakaoikosa mechi ya leo ni Diego Dalot, Eric Bailly.

Tangu ujio wa Roman Abramovich kama mmiliki mkuu wa Chelsea mnamo 2003, klabu hiyo pamoja na Manchester United zimetwaa mataji mengi kuliko timu nyingine za EPL- Chelsea 16, Manchester 14.

Hii itakuwa mara ya tano timu hizo kukutana katika Carabao Cup. Karibuni zaidi ukiwa msimu wa 2012/13, raundi ya tano.

Timu hizo zilikutana kwa mara ya kwanza msimu wa 1970/71 raundi ya nne ambapo Manchester walishinda 2-1, zikakutana tena katika hatua ya robo-fainali msimu wa 2002/03 na pia wakashinda 1-0.

Walikutana pia katika hatua ya nusu-fainali, mkondo wa kwanza na kutoka sarea 0-0, lakini Chelsea wakashinda mkondo wa pili ugenini kwa 2-1. Zilikutana kwa mara ya mwisho msimu wa 2012/13 raundi ya nne ambapo Manchester United walishinda kwa 5-4.

Kwa jumla, matokeo ya Chelsea dhidi ya Manchester katika michuano hii ni ushindi mara saba, sare mara nne na kushindwa mara 13.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana katika pambano la maondoano ilikuwa msimu uliopita, pambano la FA Cup.

Droo ya mechi za robo-fainali inatarajiwa kufanyika kesho asubuhi na kuonyeshwa moja kwa moja kwenye runinga.

Katika mechi nyingine, Aston Villa watakuwa nyumbani kucheza na Wolves, pia usiku.