Chelsea kutumia mechi yao ijayo ya EPL kuwasoma zaidi Man-City kabla ya fainali ya UEFA

Chelsea kutumia mechi yao ijayo ya EPL kuwasoma zaidi Man-City kabla ya fainali ya UEFA

Na MASHIRIKA

KOCHA Thomas Tuchel wa Chelsea amesema watatumia gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) litakalowakutanisha na Manchester City mnamo Mei 8, 2021, ugani Etihad kuwasoma zaidi wapinzani hao kabla ya fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Mei 29 jijini Istanbul, Uturuki.

Chelsea waliwakung’uta Real Madrid ambao ni mabingwa mara 13 wa UEFA 2-0 mnamo Jumatano ugani Stamford Bridge na kuwadengua kwa jumla ya magoli 3-1 kwenye nusu-fainali ya msimu huu.

Ufanisi huo uliwakatia Chelsea tiketi ya kupepetana na Man-City ya kocha Pep Guardiola kwenye fainali ya UEFA, hii ikiwa mara ya nne kwa vikosi hivyo kukutana kwenye kampeni za muhula huu wa 2020-21.

“Naridhishwa zaidi na motisha ya vijana. Wana kiu ya kutwaa ufalme wa UEFA na hili ni jambo ambalo walianza kudhihirisha wazi tangu walipotinga hatua ya 16-bora. Walikomoa Atletico Madrid na kuzamisha chombo cha FC Porto kabla ya kuwadengua Real. Kikosi kinazidi kukomaa na nahisi kwamba tunaelekea kufikia uthabiti ambao klabu kama vile Bayern Munich na Man-City wanajivunia,” akasema Tuchel.

Baada ya Man-City kuwapokeza Chelsea kichapo cha 3-1 kwenye mkondo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu Chelsea wakiwa chini ya kocha Frank Lampard, Tuchel alitua ugani Stamford Bridge na kuongoza ufufuo wa makali ya waajiri wake.

Chini ya Tuchel, Chelsea walizamisha matumaini ya Man-City kutia kapuni jumla ya mataji manne msimu huu kwa kuwapokeza kichapo cha 1-0 kilichowadengua kwenye nusu-fainali ya Kombe la FA mnamo Aprili 17, 2021, ugani Wembley, Uingereza.

Man-City watakuwa wenyeji wa Chelsea katika mkondo wa pili wa gozi la EPL mnamo Jumamosi ya Mei 8 ugani Etihad wakilenga kushinda na kutawazwa wafalme wa taji hilo kwa mara ya tatu chini ya kipindi cha misimu minne.

“Mechi hiyo itakuwa kama nusu-fainali ya UEFA. Tutajituma vilivyo na tuna matumaini tele kwamba tutashinda na kupata motisha ya kuwazamisha kwenye fainali. Mchuano huo utatupa jukwaa jingine mwafaka la kuwasoma Man-City,” akasema Tuchel.

Chelsea walikuwa wakikamata nafasi ya tisa kwenye msimamo wa jedwali la EPL wakati walipomwaminia Tuchel ambaye ni kocha wa zamani wa Borussia Dortmund na Paris Saint-Germain (PSG) kuwa mrithi wa Lampard mnamo Januari 2021.

Wakikalia nafasi ya nne kwa sasa kwenye jedwali la EPL kwa alama tatu zaidi kuliko nambari tano West Ham United, Chelsea watapepetana pia na Leicester City kwenye fainali ya Kombe la FA mnamo Mei 15 ugani Wembley, Uingereza. Fainali dhidi ya Man-City itakuwa yao ya tatu kunogesha kwenye kampeni za UEFA.

Baada ya kuzidiwa maarifa na Manchester United kwenye fainali ya 2008 jijini Moscow nchini Urusi, Chelsea waliwapiga Bayern Munich 4-3 kupitia penalti kwenye fainali ya UEFA miaka minne baadaye.

“Sasa tuko kwenye fainali mbili na muhimu zaidi kwetu ni kujinyima vilivyo na kukamilisha vibarua hivi tulivyovianza tangu siku ya kwanza,” akasema Tuchel.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Nafasi ya ukocha katika timu ya Uingereza U-21 yavutia...

Gozi la EPL lililoahirishwa kati ya Man-United na Liverpool...