Michezo

Chelsea mbioni kumnyaka juu kwa juu kocha wa Leicester Enzo Maresca

May 29th, 2024 2 min read

LONDON, Uingereza

Chelsea wanakaribia kumsajili kocha Enzo Maresca wa Leicester City kujaza nafasi ya Mauricio Pochettino aliyegura kwa hiari baada ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kumalizika.

Hii ni baada kocha Kieran McKenna kujiondoa katika vita vya kuwania nafasi hiyo.

Wengine waliokuwa wakifikiriwa kwa kazi hiyo ni Roberto de Zerbi na Thomas Frank waliokuwa makocha wa Brighton na Brentford mtawalia.

Kulingana na ripoti ya vyombo vya habari vya hapa nchini, Chelsea wanafanya harakati za haraka kufuatia kuondoka kwa Pochettino kuhakikisha raia huyo wa Italia amechukua nafasi hiyo, hata hivyo, itabidi vigogo hao wa EPL walipe Leicester City fidia ya Sh1.6 bilioni.

Akiwa na Leicester City, Maresca aliongoza timu hiyo kutwaa ubingwa wa taji la Chmpionship msimu uliopita na kuirejesha kwenye EPL, baada ya hapo awali kuwa kocha msaidizi wa Pep Guardiola katika klabu ya Manchester City.

Chelsea wanatarajiwa kumpa kocha huyo mkataba wa miaka mitano kwa mujibu wa ripoti kutoka Stamford Bridge, makao makuu ya Chelsea FC. Kulingana na taarifa za mkataba huo, Mwitaliani huyo anataka kuja na wasaidizi wake watano.

Kipa wa zamani wa Chelsea, Willy Caballero anatarajiwa kuwa miongoni mwa wasaidizi wa kocha huyo mwenye umri wa miaka 44.

Caballero alikuwa msaidizi wa Maresca katika klabu ya Leicester City kwenye idara ya yake ya kiufundi pale King Power Stadium.

Caballero alichezea Chelsea kati ya 2017 na 2021, baada ya kujiunga nao kwa uhamisho huru akitokea Manchester City na kuichezea mechi 38.

Pochettino aliondoka Stamford Bridge kwa hiari baada ya kusaidia Chelsea kumaliza katika nafasi ya sita jedwalini EPL.

Maresca aliteuliwa na wakurugenzi wa michezo, Paul Winstanley na Laurence Steward miongoni mwa makocha kadhaa waliotuma maombi.

Behdad Eghbali ambaye ni mmoja wa wamiliki wakuu wawili wa Chelsea vile vile yuko jijini hapa kushiriki katika mazungmzo ya mkataba wa Maresca.

Chelsea wanaamini Maresca ndiye anayefaa kwa kazi hiyo, kulingana na miundo ya klabu hiyo, baada ya kuvutiwa na maoni yake kuhusu kikosi cha sasa.

Utendakazi wake baada ya kufanya kazi chini ya Guardiola pia umewapa wakuu wa Chelsea matumaini makubwa kwamba atafanya kazi nzuri na kuleta ufanisi pale Stamford Bridge.

Mikel Arteta aliyeleta mabadiliko makubwa katika klabu ya Arsenal alifanya kazi chini ya Guardiola pale Etihad Stadium kabla ya kuondoka.

Chelsea wanaamini Maresca ndiye anayefaa kuongezea kikosi cha sasa mbinu zitakazoifanya timu hiyo ianze kuvuma kuanzia msimu ujao.

Aliyekuwa kocha msaidizi wa Manchester United, McKenna aliyesaidia Ipswich kurejea kwenye EPL anatarajiwa kujiunga na Brighton, au kurejea pale Old Trafford iwapo mabingwa hao wa FA Cup watamtimua Erik ten Hag.

McKenna ana mkataba wa hadi 2027 na klabu ya Ipswich ambapo klabu itakayomtaka itabidi ilipe fidia ya Sh700 milioni.