Chelsea wabomoa Spurs

Chelsea wabomoa Spurs

Na MASHIRIKA

KOCHA Jose Mourinho alisalia kumlaumu refa Andre Mariner kwa baadhi ya maamuzi yaliyochangia kikosi chake cha Tottenham Hotspur kupokezwa kichapo cha 1-0 na Chelsea katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Februari 4, 2021.

Chelsea waliendeleza rekodi yao ya kutoshindwa chini ya mkufunzi mpya Thomas Tuchel na ushindi dhidi ya Spurs uliwapaisha hadi nafasi ya sita kwenye msimamo wa jedwali la EPL.

Kufikia sasa, Chelsea wanajivunia alama 36 sawa na Everton ambao wana mechi mbili zaidi za kupiga ili kufikia idadi ya michuano ambayo imesakatwa na masogora wa Tuchel ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Borussia Dortmund na Paris Saint-Germain (PSG).

Kwa upande wao, Spurs walishuka hadi nafasi ya nane kwa pointi 33, mbili zaidi kuliko Arsenal ambao wanafunga mduara wa 10-bora.

“Namchukulia Marriner kuwa miongoni mwa marefa bora zaidi kwa sasa katika EPL. Namjali sana na ninavutiwa sana na utendakazi wake. Uhusiano huo unaniweka katika nafasi ya kumkosoa iwapo sijaridhishwa na jinsi alivyosimamia mechi,” akasema Mourinho baada ya kuonekana kuzamia kwene mazungumzo marefu na Marriner mwishoni mwa mechi.

“Mwishoni mwa mechi, ni penalti ndiyo iliamua mshindi wa mechi hiyo. Penalti yenyewe haikustahili kutolewa kabisa na ni uchungu sana kupoteza mchuano mkubwa wa sampuli hiyo.

Penalti ya Chelsea ilifumwa wavuni na kiungo Jorgino kunako dakika ya 24.

Tuchel kwa sasa amewaongoza Chelsea kusajili ushindi mara mbili na kuambulia sare mara moja bila ya kikosi chake kufungwa bao. Tangu aaminiwe kuwa mrithi wa Frank Lampard, matokeo ya Chelsea yamedhihirisha kwamba wao ni miongoni mwa wagombezi halisi wa taji la EPL msimu huu chini ya Tuchel.

“Tulidhibiti mchezo katika kipindi kizima cha kwanza. Huenda kujiamini kwetu kulipotea kidogo katika kipindi cha pili kwa sababu tulishindwa kumiliki asilimia kubwa ya mpira. Lakini hatimaye tulipata ushindi muhimu,” akaongeza Tuchel.

Kichapo kwa Spurs kilikuwa cha tatu mfululizo kwa kikosi hicho kupokezwa katika uwanja wao wa nyumbani. Kwa kuwa nahodha wao Harry Kane hakuwepo, Spurs wakisalia kumtegemea pakubwa chipukizi Carlos Vinicius katika safu ya mbele japo Serge Aurier alipoteza nafasi kadhaa za wazi ambazo zingewapa waajiri wao bao la kusawazisha. Kipa Edouard Mendy pia alipangua kirahisi makombora aliyoelekezewa na Erik Lamela na Mason Mount.

Kati ya mabadiliko makubwa yanayoendelea kutambisha Chelsea chini ya Tuchel ni maamuzi ya kocha huyo kuwajibisha Reece James na Callum Hudson-Odoi wanaozidi kushirikiana vilivyo.

Pigo la pekee kwa Chelsea baada ya mchuano huo ni jeraha la paja lililomweka beki Thiago Silva katika ulazima wa kuondolewa uwanjani mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Ni mara ya kwanza kwa Mourinho kupoteza mechi mbili kwa mpigo katika jumla ya michuano 327 ambayo amesimamia katika EPL kufikia sasa.

Tuchel ndiye kocha wa kwanza wa Chelsea baada ya Mourinho mnamo Agosti 2004 kushuhudia kikosi chake kikikosa kufungwa bao kutokana na mechi tatu za kwanza kambini mwa mabingwa hao wa EPL 2016-17.

Ilikuwa mara ya kwanza tangu Novemba 2012 kwa Spurs kupoteza mechi tatu mfululizo za EPL.

Alama saba ambazo Chelsea wamejivunia kutokana na mechi tatu chini ya Tuchel zinawiana na idadi ya pointi ambazo kikosi hicho kilijizolea kutokana na mechi nane za mwisho chini ya Lampard.

Spurs kwa sasa wanajiandaa kuwa wenyeji wa West Bromwich Albion mnamo Januari 7 huku Chelsea wakiwaendea Sheffield United uwanjani Bramall Lane.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

THIS LOVE: Wakenya wawapongeza Nameless na Wahu kwa utunzi...

CORONA: Liverpool hawawezi kusafiri Ujerumani kwa mchuano...