Michezo

Chelsea wafunga manne na kurefusha mkia wa Sheffield United kwenye jedwali la EPL

November 8th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

CHELSEA walitoka nyuma na kuwapokeza Sheffield United kichapo cha 4-1 katika mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) uliowakutanisha uwanjani Stamford Bridge mnamo Novemba 7, 2020.

Ushindi wa Chelsea ulisaza Sheffield United ya kocha Chris Wilder kwenye mkia wa jedwali la EPL ikizingatiwa kwamba kikosi hicho hakijasajili ushindi wowote kutokana na mechi nane zilizopita ambazo zimekishuhudia kikipoteza mara saba na kusajili sare mara moja.

David McGoldrick aliwaweka Sheffield United almaarufu ‘The Blades’ uongoni katika dakika ya tisa kabla ya Tammy Abraham kusawazisha kunako dakika ya 23. Mabao mengine ya Chelsea yalifumwa wavuni kupitia kwa Ben Chilwell, Thiago Silva na Timo Werner.

Huku Sheffield United wakivuta mkia kwa alama moja pekee kutokana na mechi nane, Chelsea walipaa hadi nafasi ya tatu kwa alama 15.

Mbali na goli la Abraham, mabao mengine matatu ya Chelsea yalifumwa wavuni na sajili wapya waliotua uwanjani Stamford Bridge msimu huu – Chilwell, Silva na Werner. Hakim Ziyech ambaye pia alijiunga na Chelsea msimu huu, aliridhisha pakubwa na kuchangia mabao mawili ya waajiri wake.

Kwa kuwa EPL inaingia likizo fupi kwa minajili ya kupisha mechi za kimataifa, ina maana kwamba Sheffield United watasalia mkiani mwa jedwali kwa kipindi cha siku 14 zijazo baada ya kupoteza mechi zote za mwezi mmoja uliopita dhidi ya Liverpool, Arsenal, Man-City na Chelsea. Mechi zijazo za Sheffield United zitakuwa dhidi ya West Ham United na West Bromwich Albion.

Chelsea kwa sasa wamepoteza mechi moja pekee kati ya sita zilizopita dhidi ya Sheffield United ligini. Hata hivyo, ushindi wa Novemba 7 ulikuwa wao wa kwanza dhidi ya The Blades katika EPL tangu Machi 2007.

Rekodi ya Chelsea ya kutoshindwa kwenye mechi 11 zilizopita ndiyo ndefu zaidi kwa kikosi hicho tangu Novemba 2018 ambapo walipiga jumla ya michuano 18 bila kupoteza hata moja.

Kwa upande wao, rekodi ya Sheffield United ya kutoshinda mechi yoyote kati ya 12 zilizopita ndiyo ndefu zaidi kwa kikosi hicho tangu Oktoba 2013. Chelsea kwa sasa wanajiandaa kuwaendea Newcastle United uwanjani St James’ Park kwa gozi jingine la EPL mnamo Novemba 21, 2020.