Chelsea walipiza kisasi dhidi ya Leicester City na kujiweka pazuri kufuzu kwa UEFA msimu ujao

Chelsea walipiza kisasi dhidi ya Leicester City na kujiweka pazuri kufuzu kwa UEFA msimu ujao

Na MASHIRIKA

CHELSEA waliimarisha nafasi yao ya kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula ujao kwa kuwapokeza Leicester City kichapo cha 2-1 mnamo Jumanne usiku.

The Blues walisajili ushindi huo siku tatu baada ya Leicester kuwakomoa 1-0 kwenye fainali ya Kombe la FA uwanjani Wembley, Uingereza. Antonio Rudiger na Jorginho walifunga magoli yaliyowezesha Chelsea kulipiza kisasi dhidi ya Leicester mbele ya takriban mashabiki 8,000 uwanjani Stamford Bridge.

Huku Chelsea wakipaa hadi nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 67, Leicester wanaojivunia alama 66 walishuka hadi nafasi ya nne na kwa sasa wako katika hatari ya kupitwa na Liverpool watakaovaana na Burnley mnamo Mei 19, 2021 ugani Turf Moor. Liverpool ya kocha Jurgen Klopp inakamata nafasi ya tano jedwalini kwa pointi 63.

Ingawa Kelechi Iheanacho alipania kurejesha Leicester mchezoni katika kipindi cha pili, bao lake la dakika ya 76 halikutosha kuwateteresha Chelsea waliosalia imara katika safu yao ya ulinzi.

Baada ya Rudiger kufungulia Chelsea ukurasa wa mabao katika dakika ya 47, kikosi hicho cha kocha Thomas Tuchel kilipata goli la pili kupitia penalti baada ya Wesley Fofana kumwangusha fowadi Timo Werner ndani ya kijisanduku.

Ni matarajio ya Tuchel kwamba ushindi wao dhidi ya Leicester ligini utawapa vijana wake motisha zaidi ya kuangusha Manchester City kwenye fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) itakayowakutanisha mnamo Mei 29, 2021 jijini Porto, Ureno.

Ushindi kwa Chelsea dhidi ya Aston Villa katika mchuano wa mwisho msimu huu ligini mnamo Mei 23 utawapa uhakika wa kukamilisha kampeni ndani ya mduara wa nne-bora na kufuzu kwa soka ya UEFA muhula ujao hata iwapo watazidiwa maarifa na Man-City kwenye fainali.

Leicester wamejipata katika mtihani mgumu wa kuepuka masaibu ya msimu wa 2019-20 uliowashuhudia wakipoteza fursa ya kufuzu kwa soka ya UEFA katika siku ya mwisho licha ya kuwa ndani ya orodha ya nne-bora kwa kipindi kirefu kwenye kampeni za muhula huo.

Chini ya kocha Brendan Rodgers, Leicester watafunga rasmi kampeni za msimu huu dhidi ya Tottenham Hotspur mnamo Mei 23. Kufuzu kwao kwa kivumbi cha UEFA muhula ujao kutategemea matokeo watakayosajili dhidi ya Spurs na yale yatakayosajiliwa na Liverpool dhidi ya Burnley na Crystal Palace katika mechi mbili zijazo.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Guardiola ataka Manchester City kujinyanyua upesi na...

Manchester United wakabwa koo na Fulham katika EPL uwanjani...