Michezo

Chelsea wapepeta Newcastle na kupaa hadi kileleni mwa jedwali la EPL

November 21st, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

CHELSEA walipaa hadi kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Novemba 21, 2020 baada ya kuwapepeta Newcastle United 2-0 uwanjani St James’ Park.

Ushindi huo wa Chelsea ulikuwa wao wa tano mfululizo katika mashindano yote ya msimu huu.

Federico Fernandez alijifunga katika ya 10 baada ya kushindwa kuhimili presha kutoka beki Ben Chilwell na kuwapa Chelsea motisha zaidi ya kumiliki asilimia kubwa ya mpira na kutamalaki mchuano.

Chelsea wangalifunga idadi kubwa zaidi ya mabao katika kipindi cha pili ila wakanyimwa fursa hizo na kipa wa Newcastle, Karl Darlow aliyepangua makombora mazito aliyoelekezewa na Timo Werner na Tammy Abraham.

Hata hivyo, Abraham alihakikisha kwamba wanatia kapuni alama zote tatu kutokana na mechi hiyo baada ya kukamilisha kwa ustadi krosi ya Werner katika dakika ya 65. Isaac Hayden, Joelinton de Lira na Sean Longstaff ni miongoni mwa wanasoka wa Newcastle waliotia fora zaidi katika mechi hiyo.

Chelsea, walioanza mchuano wakiwa kileleni mwa jedwalini, sasa wanajivunia alama sawa na Leicester City (18) ambao watakuwa wageni wa Liverpool ugani Anfield mnamo Novemba 22, 2020.

Licha ya kuongoza kundi lao katika Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), Chelsea kwa sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali la EPL kwa mara ya kwanza tangu kocha Frank Lampard aaminiwe fursa ya kudhibiti mikoba yao mnamo 2019.

Mchuano huo ulikuwa wa kwanza kati ya tisa ijayo ambayo Chelsea watalazimika kupiga chini ya kipindi cha wiki nne bila ya huduma za wanasoka matata zaidi waliorejea katika nchi zao kwa mechi za kimataifa.

Lampard alimwajibisha beki Antonio Rudiger katika nafasi ya difenda Thiago Silva, 36, aliyekuwa sehemu ya kikosi kilichotegemewa na Brazil katika mechi zilizopita za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.