Chelsea wapewa Man-City huku Leicester wakionana na Southampton kwenye nusu-fainali za Kombe la FA

Chelsea wapewa Man-City huku Leicester wakionana na Southampton kwenye nusu-fainali za Kombe la FA

Na MASHIRIKA

MABINGWA mara nane wa Kombe la FA, Chelsea, watakwaruzana na Manchester City kwenye nusu-fainali za Kombe la FA msimu huu wa 2020-21.

Leicester City kwa upande wao watavaana na Southampton huku mechi zote mbili zikiratibiwa kusakatiwa uwanjani Wembley, Uingereza mnamo Aprili 17 na 18, 2021.

Chelsea ambao walipigwa 2-1 na Arsenal kwenye fainali ya 2019-20, walitinga hatua ya nne-bora msimu huu baada ya kuwapokeza Sheffield United kichapo cha 2-0 kwenye robo-fainali za Jumapili usiku.

Kwa upande wao, Leicester hawajawahi kushinda Kombe la FA baada ya kuzidiwa maarifa mara nne kwenye fainali. Wanasoka hao wa kocha Brendan Rodgers walifuzu kwa nusu-fainali za muhula huu baada ya kuwadengua Manchester United kwa kichapo cha 3-1 mnamo Jumapili usiku uwanjani King Power.

Southampton ya kocha Ralph Hasenhuttl walijikatia tiketi ya nusu-fainali baada ya kuwapiga AFC Bournemouth 3-0 mnamo Machi 20, 2021 uwanjani Vitality huku Man-City ya mkufunzi Pep Guardiola ikiwacharaza Everton 2-0 ugani Goodison Park.

Fainali ya Kombe la FA muhula huu itapigiwa uwanjani Wembley mnamo Mei 15, 2021 na huenda ikahudhuriwa na zaidi ya mashabiki 20,000.

Ushindi uliosajiliwa na Chelsea dhidi ya Sheffield United uliendeleza rekodi ya kutoshindwa kwa kocha Thomas Tuchel katika jumla ya mechi 14 tangu aaminiwe kuwa mrithi wa kocha Frank Lampard uwanjani Stamford Bridge.

Man-City ambao wanafukuzia mataji manne msimu huu, walifungiwa mabao yao mawili yaliyodengua Everton kupitia viungo Ilkay Gundogan na Kevin de Bruyne.

Nathan Redmond alifungia Southampton mabao mawili na kuchangia moja jingine katika ushindi wa 3-0 uwanjani Vitality. Leicester watakutana na Southampton almaarufu The Saints wakijivunia motisha ya kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 9-0 dhidi ya kikosi hicho katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2019-20 uwanjani St Mary’s.

DROO YA NUSU-FAINALI ZA KOMBE LA FA

Leicester City na Southampton

Chelsea na Manchester City

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Arsenal watoka nyuma kwa mabao matatu na kuwalazimishia...

KCPE yaanza kwa visa vya kujifungua