Michezo

Chelsea watinga Uefa msimu ujao huku Wolves wakikosa fursa ya kufuzu kwa Europa League moja kwa moja

July 27th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

CHELSEA walikamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu wa 2019-20 katika nafasi ya nne jedwalini na kujikatia tiketi ya kushiriki soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula ujao baada ya kuwapepeta Wolves 2-0 uwanjani Stamford Bridge mnamo Jumapili.

Wanasoka hao wa kocha Frank Lampard walijibwaga ugani kwa minajili ya mechi hiyo wakihitaji alama moja pekee dhidi ya Wolves ili kujipa uhakika wa kufunga orodha ya nne-bora kileleni mwa jedwali la EPL. Hata hivyo, walijikuta wakitamba zaidi dhidi ya Wolves ambao kwa sasa wamekosa tiketi ya moja kwa moja ya kushiriki Europa League msimu ujao.

Mason Mount alifunga bao mwishoni mwa kipindi cha kwanza, sekunde chache kabla ya mshambuliaji wa zamani wa Arsenal, Olivier Giroud kufunga la pili na kuwanyamazisha kabisa Wolves ambao waliambulia nafasi ya saba kwa alama 59 sawa na Tottenham Hotspur walioorodheshwa mbele yao kutokana na wingi wa mabao. Goli la Giroud ambaye ni mzawa wa Ufaransa, lilikuwa lake la saba kati ya mechi nane zilizopita.

Tottenham ya kocha Jose Mourinho ililazimishiwa sare ya 1-1 na Crystal Palace uwanjani Selhurst Park.

Wolves watafuzu sasa kwa Europa League msimu ujao iwapo Chelsea watawacharaza Arsenal kwenye fainali ya Kombe la FA ambayo imepangiwa kuwakutanisha mnamo Agosti 1, 2020 uwanjani Wembley, Uingereza.

Chelsea walikamilisha kampeni zao za EPL msimu kwa alama 66, sawa na Manchester United waliowapepeta Leicester City 2-0 uwanjani King Power na kupaa hadi nafasi ya tatu kwa wingi wa mabao.

Licha ya kunyanyua ubingwa wa Europa League msimu uliopita wa 2019-20 na kuambulia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la EPL, Chelsea walimfuta kazi kocha Maurizio Sarri na kumpokeza mikoba mchezaji wao wa zamani Frank Lampard aliyekuwa akiwatia makali vijana wa Derby County wanaoshiriki Ligi ya Daraja la Kwanza nchini Uingereza (Championship). Sarri kwa sasa anadhibiti mikoba ya Juventus nchini Italia.

Chelsea wanatazamiwa kutamba zaidi katika kampeni za muhula ujao hasa ikizingatiwa kwamba tayari wamejitwalia huduma za mshambuliaji Timo Werner na kiungo Hakim Ziyech kutoka RB Leipzig (Ujerumani) na Ajax (Uholanzi) mtawalia. Kikosi hicho cha Lampard kinatazamiwa pia kujinasia huduma za fowadi Kai Havertz kutoka Bayer Leverkusen ya Ujerumani.