Michezo

Chelsea watoka sare ya 3-3 dhidi ya West Bromwich Albion

September 26th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

TAMMY Abraham alifunga bao la kusawazisha mwishoni mwa kipindi cha pili na kuzolea Chelsea alama moja baada ya kuambulia sare ya 3-3 dhidi ya West Bromwich Albion mnamo Septemba 26, 2020.

Kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza, Chelsea walikuwa nyuma kwa mabao 3-0 katika gozi hilo lililosakatiwa ugani The Hawthorns.

Chini ya kocha Frank Lampard, Chelsea nusura wapoteze mechi yao ya pili mfululizo ligini baada ya chombo chao kuzamishwa kwa kichapo cha 2-0 kutoka kwa Liverpool uwanjani Stamford Bridge mnamo Septemba 20.

West Brom walifunga mabao matatu ya haraka chini ya dakika 30 za kwanza. Masihara ya beki Marcos Alonso katika dakika ya nne yaliwapa West Brom fursa ya kufunga kupitia kwa Callum Robinson aliyeshirikiana vilivyo na Matheus Pereira.

Kocha Frank Lampard ambaye aliashiria dalili za kupoteza imani kwa kipa Kepa Arrizabalaga dhidi ya Liverpool, alimwajibisha kipa mkongwe Willy Caballero, 38, michumani dhidi ya West Brom.

Kosa la sajili mpya wa Chelsea katika safu ya nyuma Thiago Silva, lilichangia bao la pili la West Brom lilifumwa wavuni na Robinson katika dakika ya 25 kabla ya Kyle Bartley kufanya mambo kuwa 3-0 katika dakika ya 27.

Chelsea walirejelea kampeni za kipindi cha pili wakiwa ‘simba majeruhi’ na wakafunga bao la kwanza kunako dakika ya 55 kupitia kwa chipukizi Mason Mount.

Callum Hudson-Odoi alitokea benchi katika dakika ya 60 na kuongeza kasi katika safu ya mbele ya Chelsea. Mwingereza huyo alifunga bao la pili la Chelsea katika dakika ya 70 na kuamsha motisha zaidi ya waajiri wake.

Abraham aliwaepushia aibu ya kupigwa katika mechi ya pili mfululizo mwanzoni mwa msimu wa EPL katika dakika ya 90 kwa kuvurumisha fataki langoni mwa West Brom baada ya kombora la Mount kupanguliwa na kipa.

Chelsea walianza vyema kampeni za msimu huu kwa kuwapiga Brighton 3-1 uwanjani Amex mnamo Septemba 14, 2020.

Kikosi hicho kimetumia zaidi ya Sh35 bilioni kujisuka upya msimu huu na wamesajili wanasoka sita wakiwemo Timo Werner, Kai Harvertz, Hakim Ziyech, Xavier Mbuyamba, Malang Sarr, Ben Chilwell, Silva na kipa Edouard Mendy.

Katika mahojiano yaka na wanahabari mwishoni mwa mechi hiyo, Lampard alifichua kwamba kikosi chake kinakaribia kujinasia huduma za kipa Edouard Mendy kutoka Rennes ili awe kizibo cha Arrizabalaga ambaye kwa sasa ni kipa ghali zaidi duniani.