Michezo

Chelsea wavunja benki na kumsajili beki Ben Chilwell kutoka Leicester

August 27th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

CHELSEA wamemsajili beki mzawa wa Uingereza, Ben Chilwell kwa mkataba wa miaka mitano kutoka Leicester City.

Uhamisho wa nyota huyo umerasimishwa kwa kima cha Sh6.3 bilioni.

Cheilwell anakuwa mchezaji wa tatu kusajiliwa na Chelsea muhula huu baada ya kikosi hicho cha kocha Frank Lampard kujinasia pia huduma za fowadi Hakim Ziyech, 27, kutoka Ajax ya Uholanzi na mshambuliaji Timo Werner, 24, aliyeagana rasmi na RB Leipzig ya Ujerumani.

Chilwell, 23, alipokezwa malezi ya awali kabisa ya kusakata soka katika akademia ya Leicester ugani King Power. Aliwajibishwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha watu wazima mnamo 2015 na hadi kuondoka kwake, alikuwa na miaka minne zaidi kwenye mkataba wake na Leicester.

Sogora huyo hakuwa sehemu ya kikosi cha Leicester kilichotegemewa na kocha Brendan Rodgers kwenye mechi za mwisho za msimu huu wa 2019-20 kutokana na jeraha la mguu.

Chini ya Lampard, Chelsea walikamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu katika nafasi ya nne, mbele ya Leicester waliopigiwa upatu wa kufuzu kwa kivumbi cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula ujao.

“Nimekuwa nikitazamia sana kuwa sehemu ya kikosi hiki kichanga kinachoundwa na Lampard. Kubwa zaidi katika maazimio yangu ni kuongoza klabu kutwaa mataji mengi zaidi iwezekanavyo katika kampeni za msimu ujao,” akasema Chilwell ambaye anajivunia kuchezeshwa na timu ya taifa ya Uingereza mara 11.

Hadi alipoagana na Leicester, Chilwell alikuwa amevalia jezi za kikosi hicho mara 123 na kukifungia jumla ya mabao manne, matatu kati ya magoli hayo yalitokana na kivumbi cha EPL msimu huu wa 2019-20.

Chilwell anaungana sasa kambini mwa Chelsea na wanasoka Danny Drinkwater na N’Golo Kante waliowahi kucheza pamoja naye katika kikosi cha Leicester.

Kante alisajiliwa na Chelsea kutoka Leicester mnamo 2016 kabla ya Drinkwater kumfuata mnamo 2017. Riyad Mahrez aliagana pia na Leicester mnamo 2018 na kutua uwanjani Etihad kuvalia jezi za Manchester City huku Harry Maguire akiyoyomea Manchester United mnamo 2019.

Mazoea haya ya Leicester ya kuuza mchezaji wao nyota kila mwaka ni biashara ambayo inawastawisha vyema kiuchumi. Wanasoka hawa watano waliuzwa na Leicester kwa kima cha Sh35 bilioni baada ya kuwanunua wote kwa jumla ya Sh3.3 bilioni pekee.

Licha ya kuagana na sogora nyota na tegemeo kila msimu kwa mfululizo wa miaka mitano iliyopita, Leicester bado walifaulu kukamilisha kampeni zao za msimu wa 2019-20 mbele ya Arsenal na Tottenham Hotspur kwenye jedwali la EPL.