Michezo

Chelsea yaendelea kupuuza Sterling


HALI ya baadaye ya Raheem Sterling katika klabu ya Chelsea imo shakani baada ya jina la kiungo huyo mshambuliaji kukosekana katika kikosi kitakachocheza na Servette ya Uswisi Alhamisi, Agosti 22, 2024 katika mechi ya mchujo wa Europa Conference League, mkondo wa kwanza itakayochezewa Stamford Bridge.

Nyota huyo vile vile aliikosa mechi ya ufunguzi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) dhidi ya Manchester City mwishoni mwa wiki baada ya kocha Enzo Maresca kumpuuza kufuatia madai kwamba alikuwa mpango wa kuondoka klabuni na kujiunga na klabu ya Juventus nchini Italia.

Mbali na Juventus, kuna uvumi kwamba West Ham United na Crystal Palace ni miongoni mwa klabu zinazopigania saini ya Muiingereza huyo mwenye umri wa miaka 29.

Sterling ameichezea Chelsea mechi 18 tangu ajiunge nao akitokea Manchester City kwa kitita cha Sh8.3 bilioni mnamo Julai 2022.

Wachezaji wengine wa Chelsea watakaoikosa mechi ya kesho dhidi ya Servette ni walinzi Ben Chiwell, Wesley Fofana na Tosin Adarabioyo.

Chelsea imetumia kiasi cha Sh30.9 bilioni kununua wachezaji 11 msimu huu wa usajili wa kiangazi, huku kukiwa na madai kwamba amechanganyikiwa na idadi kubwa ya wachezaji 40 wa kikosi cha kwanza.