Chelsea yaibuka Klabu Bora ya Mwongo kati ya 2011 na 2020

Chelsea yaibuka Klabu Bora ya Mwongo kati ya 2011 na 2020

Na MASHIRIKA

CHELSEA wametawazwa kuwa Kikosi Bora cha Mwongo katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Haya ni kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Historia na Takwimu za Soka (IFFHS) ambalo limekuwa likitathmini maendeleo ya vikosi vyote vya soka duniani katika kipindi cha miaka 10 iliyopita kati ya 2011 na 2020.

Kwa mujibu wa IFFHS, Barcelona inayoshiriki Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) ndiyo Klabu Bora ya Mwongo Duniani.

Chelsea almaarufu ‘The Blues’ waliibuka washindi wa mataji ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2014-15 na 2016-17.

Aidha, walijinyakulia ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2012 walipowapepeta miamba wa Ujerumani, Bayern Munich kwenye fainali iliyoandaliwa uwanjani Allianz Arena.

Ni katika msimu uo huo ambapo Chelsea pia walijizolea ubingwa wa Kombe la FA kabla ya kujitwalia taji hilo kwa mara nyingine mnamo 2018, miaka mitatu baada ya kutawazwa mabingwa wa League Cup mnamo 2015.

Katika kipindi cha mwongo mmoja uliopita, Chelsea waliongozwa pia na wakufunzi Rafael Benitez na Maurizio Sarri kutwaa mataji mawili ya Europa League.

Hata hivyo, Chelsea waliwaduwaza wengi kwa kuambulia nafasi ya 10 kwenye kampeni za EPL mnamo 2015-16 kabla ya kujinyanyua msimu uliofuata na kutia kapuni ubingwa wa EPL.

Klabu iliyoambulia nafasi ya pili kwenye orodha ya IFFHS miongoni mwa vikosi vya Uingereza ni Manchester City waliojizolea mataji manne ya EPL. Wakufunzi Roberto Mancini na Manuel Pellegrini walishindia kikosi hicho taji moja kila mmoja mnamo 2012 na 2014 kabla ya Pep Guardiola kuzoa mataji ya EPL mnamo 2018 na 2019.

Man-City pia walishinda Kombe la FA mnamo 2011 na 2019 huku wakitawazwa wafalme wa League Cup mara nne chini ya kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Ingawa Man-City hawajawahi kujinyanyua taji la UEFA, kikosi hicho kinajivunia kutinga nusu-fainali za kipute hicho mara moja na kinafukuzia jumla ya mataji manne kwenye kampeni za muhula huu wa 2020-21.

Manchester United waliambulia nafasi ya tatu licha ya kujishindia mataji mawili pekee ya EPL katika misimu ya mwisho ya kocha Alex Ferguson uwanjani Old Trafford.

Man-United almaarufu ‘The Red Devils’ walishinda Kombe la FA mnamo 2016 pamoja na kujizolea ufalme wa League Cup na Europa League mnamo 2017.

Arsenal waliorodheshwa katika nafasi ya nne, mbele ya Tottenham Hotspur, licha ya kutokamilisha kampeni za EPL ndani ya mduara wa nne-bora tangu 2016. Hata hivyo, kikosi hicho kinachonolewa sasa na kocha Mikel Arteta, kinajivunia kutia kibindoni mataji mengi ya Kombe la FA chini ya kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Spurs walishikilia nafasi ya tano, mbele ya Liverpool ambao ni mabingwa watetezi wa taji la EPL. Chini ya mkufunzi Jurgen Klopp, Liverpool walikung’uta Spurs mnamo 2018 na kutia kapuni taji la UEFA. Miamba hao walijizolea pia taji la League Cup mnamo 2012.

Everton ambao ni watani wakubwa wa Liverpool jijini Merseyside, waliambulia nafasi ya saba.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Klabu ya Lazio yatozwa faini na rais wake kupigwa marufuku...

Kadha wanusurika kifo baada ya basi kupoteza mwelekeo Thika...