Michezo

Chelsea yapepeta Crystal Palace 4-0

October 3rd, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

SAJILI mpya wa Chelsea, Ben Chilwell alifunga bao na kuchangia jingine katika mchuano wake wa kwanza katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) uliowakutanisha na Crystal Palace uwanjani Stamford Bridge mnamo Oktoba 3, 2020.

Mwanasoka huyo raia wa Uingereza, alisajiliwa na Chelsea kutoka Leicester City kwa kima cha Sh6.3 bilioni mnamo Agosti 27, 2020.

Chilwell alikuwa sehemu ya kikosi kilichotegemewa na kocha Frank Lampard katika ushindi wa 5-4 uliosajiliwa na Chelsea dhidi ya Tottenham katika Carabao Cup kupitia penalti mnamo Septemba 29.

Mechi ya jana ilikuwaya 100 kwa Chilwell kutandaza katika EPL. Beki huyo wa kushoto aliwafungulia Chelsea ukurasa wa mabao katika dakika ya 50 baada ya kuchuma nafuu kutokana na masihara ya beki Mamadou Sakho.

Chilwell, 23, alichangia bao la pili lililojazwa kimiani na Kurt Zouma katika dakika ya 66 kabla ya Jorge Jorginho Luiz kufunga mikwaju miwili ya penalti chini ya kipindi cha dakika nne mwishoni mwa kipindi cha pili.

Lampard alimwajibisha pia kipa mpya Edouard Mendy aliyesajiliwa kwa Sh3 bilioni kutoka Rennes kwa mara ya kwanza katika EPL.

Idara ya nyuma ya Chelsea ambao hawakufungwa kwa mara ya kwanza msimu huu, ilikuwa chini ya ulinzi wa sajili mpya Thiago Silva aliyeagana na Paris Saint-Germain (PSG) mwishoni mwa msimu uliopita.

Wanasoka wengine waliomfanyia kipa Vicente Guaita wa Palace kazi ya ziada katika mchuano huo ni Timo Werner na Tammy Abraham aliyetikisa nyavu za Palace katika mechi mbili za awali zilizoshuhudia Chelsea wakisajili ushindi wa 2-0 uwanjani Stamford Bridge kisha 3-2 ugani Selhurst Park msimu jana.

Chelsea walijibwaga ugani wakitawalia na kiu ya kujinyanyua baada ya kulazimishiwa sare ya 3-3 kutoka kwa limbukeni West Bromwich Albion katika mchuano uliotangulia wa EPL.

Ushindi dhidi ya Palace unatazamiwa sasa kuamsha motisha zaidi ya Chelsea ambao walimwaga sokoni zaodo ya Sh35 bilioni kwa minajili ya huduma za wanasoka wapya muhula huu.

Chelsea kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Southampton, Manchester United na Burnley ligini. Hadi watakaposhuka dimbani kupepetana na Burnley, Chelsea watakuwa wamekabiliana na Sevilla na Krasnodar katika gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Oktoba 20 na 28 mtawalia.

Kwa upande wao, Palace watakuwa na kibarua dhidi ya Brighton, Fulham na Wolves katika msururu wa mechi tatu zijazo.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO