Chelsea yavunja rekodi kusajili Enzo kwa Sh16.3 bilioni

Chelsea yavunja rekodi kusajili Enzo kwa Sh16.3 bilioni

NA MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

REKODI ya uhamisho kwenye Ligi Kuu ya Premia (EPL) ilivunjwa dakika ya mwisho baada ya klabu ya Chelsea kutumia kiasi cha Sh16.3 bilioni kusajili Enzo Fernandez, raia wa Argentina mwenye umri wa miaka 22.

Mkataba wa nyota huyo umevunja rekodi ya Manchester City ambao walitumia Sh15.3 bilioni kusajili Jack Grealish mnamo 2021.

Usajili wa staa huyo mwenye umri wa miaka 22 vile vile ni wa sita wenye bei ghali zaidi sawa na kiasi ambacho Barcelona ilitumia kupata huduma za mshambuliaji Antoine Griezmann mnamo 2019.

Fernandez atakayekaa Stamford Bridge hadi 2031 alisajiliwa dakika ya mwisho kabla ya dirisha la uhamisho kufungwa rasmi usiku wa manane usiku wa kuamkia jana Jumatano.

Kwa jumla, takribani Sh85 bilioni zimetumika katika shughuli za uhamisho kwenye ligi hiyo maarufu, kiasi ambacho kimevunja rekodi ya awali ya Sh66 bilioni.

Staa huyo kutoka klabu ya Benfica nchini Ureno aliibuka Mchezaji Bora Chipukizi wa Kombe la Dunia baada ya kusaidia Argentina kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia nchini Qatar, mwaka 2022.

Chelsea wamesemekana kufanya usajili huo wa nguvu kwa ajili ya kurejesha makali yake, wakati huu wanapigania vikali kutoka nafasi ya 10 wakilenga kumaliza katika Nne Bora.

Wachezaji wengine walionunuliwa na Chelsea kutoka kwa kitita cha Sh30.7 bilioni kilichotolewa na mmiliki mkuu wa klabu hiyo, Todd Boehly ni pamoja na Benoit Badiashile, Andrey Santos, Joao Felix (kwa mkopo), Noni Madueke na Mykahilo Mudryk, wengi wao wakiwa na mikataba mirefu.Miongoni mwa wachezaji walioondoka ni pamoja na Jorginho na Hakim Ziyech, wakati Mholanzi Cody Gakpo kutoka PSV akiyoyomea Liverpool.

Newcastle United imepata Anthony Gordon kutoka Everton wakati Leadro Trossard kutoka Brighton akijiunga na Arsenal.

Timu nyingi zilizokabiliwa na changamoto msimu huu zikisajili wachezaji katika juhudi za kujaribu kuimarisha vikosi vyao. Katika uhamisho huo ni pamoja na Wout Weghorst aliyejiunga na Manchester United akitokea Burnley.

Wolves chini ya mkufunzi Julen Lopetegui imefanikiwa kushajili washambuliaji Matheus Cunha na Pablo Sarabia, pamoja na kiungo Mario Lemina na beki mahiri Graig Dawson.

Nottingham Forest inayoendelea kusuasua imesajili jumla ya wachezaji 23, wakati viungo Danilo na Gustavo Scarpa na mshambuliaji Chris Wood wakijiunga na Manchester City.

Leeds United wamevunja rekodi yao ya usajili baada ya kumvutia mshambuliaji Georginio Rutter na kiungo Mwamerika Weston McKennie kutoka Juventus kwa mkopo.

Bournemouth imepata Dango Quattara, West Ham United imemnasa Dany Ings, wakati Southampton ikisajili Mislav Orsis na Carlos Alcaraz.

Kwenye shughuli hiyo, Everton ambayo majuzi ilitengana na Frank Lampard imepoteza Gordon pamoja na Arnaut Danjuma. Kiungo Naoirou Ahamada kutoka Stuttgart amejiunga na Crystal Palace, wakati kiungo Jonjo Shelvey wa Newcastle United akihamia Nottingham Forest.

  • Tags

You can share this post!

NGUVU ZA HOJA: Lugha ya Kiswahili ina uwezo wa kuimarisha...

Tume yapendekeza polisi waendelee kuvalia sare za zamani

T L