Habari Mseto

Chelugui awahakikishia Wakenya wanaohangaika kwamba wataendelea kusaidiwa

June 9th, 2020 1 min read

Na WINNIE ATIENO

WAZIRI wa Leba Simon Chelugui amewahakikishia Wakenya ambao walipoteza ajira kutokana na janga la corona kwamba wataendelea kusaidiwa.

Bw Chelugui alisema Jumatatu kwamba wafanyakazi wengi waliosimamishwa kazi kutokana na athari za janga la corona wanatoka katika sekta ya kilimo, utalii na usafiri wa ndege.

“Kafyu imewekwa ili kukabili kuenea kwa virusi hivi lakini kwa upande mwingine hatua hiyo imesababisha wengi kupoteza ajira katika sekta kadhaa. Tunabaini zaidi ya watu 1.2 milioni wamepoteza ajira. Kwa sasa mambo si mazuri, sekta kadhaa zimetangaza kusitisha ajira kwa Wakenya wengi. Inaonekana idadi ya watu wanaosimamishwa kazi inaendelea kuongezeka,” alisema Bw Chelugui.

Hata hivyo, waziri alihakikishia Wakenya kwamba kuna mikakati inayoendelea kuwekwa kusaidia wale waliopoteza ajira ili waweze kujimudu.

Alisema wizara yake inashirikiana na waajiri na sekta mbalimbali kuandika majina ya wale waliopoteza ajira na wanahitaji misaada.

“Tunaunda orodha ya waliosimamishwa kazi ili waweze kunufaika na fedha za mfuko wa Covid-19 Fund. Zaidi ya wafanyiakazi 50,000 ambao walisitishwa kazi watasaidiwa ili wajimudu,” alisema Bw Chelugui.

Waziri huyo alisema wizara hiyo inatumia Sh300 milioni kusaidia Wakenya wanaohangaika kutokana na janga la corona.

“Tulizipa kipaumbele kaunti ambazo zilifungwa kama Mombasa, Nairobi, Kwale na Kilifi. Chukulia mfano wa Mombasa ambapo wafanyakazi wengi wa wanatoka Kilifi na Kwale. Jijini Nairobi tumekuwa tukilenga mitaa duni kama Kibera, Mathare na Korogocho. Zaidi ya nyumba 108,000 zimenakiliwa wakiendelea kupata msaada wa fedha kila wiki,” alieleza Bw Chelugui.