Michezo

Chemelil, Rangers na Zoo sasa ni roho mkononi katika ligi

May 28th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

BAADA ya Vihiga United kuwa mwathiriwa wa pili kuangukiwa na shoka kwenye Ligi Kuu, macho yanaelekezwa kwa Posta Rangers, Zoo na Chemelil Sugar ambao bado wako katika vita vikali kuepuka kutemwa.

Vihiga iliungana na Mount Kenya United baada ya kumaliza msimu wake wa pili kwenye Ligi Kuu katika nafasi ya 17 ilipolemewa 2-1 na Western Stima, Jumapili.

Ikisalia mechi moja, Rangers na Zoo ziko bega kwa bega kwa alama 32 katika nafasi za 14 na 15 mtawalia, alama moja mbele ya nambari 16 Chemelil Sugar.

Rangers itazuru Tusker katika siku ya mwisho hapo Jumatano ikiwa na ufahamu itamaliza katika nafasi ya 16 isipochapa wanamvinyo hawa nao Zoo na Chemelil washinde mechi zao dhidi ya KCB na SoNy Sugar mtawalia.

Hata hivyo, hali ilivyo sasa ni Chemelil iko katika hatari zaidi ya kukutana na mmoja kutoka orodha ya Kisumu All Stars, Nairobi Stima, Ushuru, Kenya Police, Bidco United na FC Talanta zinazoweza kumaliza Ligi ya Supa katika nafasi ya tatu kufahamu hatima yake.

Chemelil, ambayo haina ushindi katika mechi nane zilizopita msimu huu, haijashinda SoNy katika mechi nne zilizopita.

Baada ya mechi za raundi ya 33 za Ligi Kuu, Gor Mahia inaongoza jedwali kwa alama 71. Mabingwa hawa mara 18 wako alama nane mbele ya Bandari ambao hawajasonga kutoka nafasi ya pili.

Washindi wa mwaka 2009 Sofapaka na mwaka 2006 SoNy wamekwamilia katika nafasi za tatu na nne kwa alama 59 na 56, mtawalia.

Sare

Gor, Bandari, Sofapaka na SoNy waliandikisha sare dhidi ya Rangers, Sofapaka, Bandari na Nzoia Sugar mtawalia wikendi iliyopita.

Mabingwa wa mwaka 2008 Mathare United na washindi mara 11 Tusker wameruka juu nafasi moja kila mmoja na kutua katika nafasi ya tano na sita kwa alama 54 na 53, mtawalia.

Mathare ilizima Chemelil 1-0 nayo Tusker ikapepeta mabingwa mara 13 AFC Leopards 2-0 kupata ufanisi huo.

Kakamega Homeboyz, ambayo mchezaji wake Allan Wanga anaongoza ufungaji wa mabao baada ya kucheka na nyavu mara 19, imeteremka nafasi mbili hadi nambari saba.

Homeboyz imezoa alama 52, pointi 12 juu ya KCB ambayo imekwamilia nafasi ya nane baada ya kulazimisha sare ya 2-2 dhidi ya Ulinzi Stars.

Ulinzi na Kariobangi Sharks, ambayo ilikung’uta Mount Kenya 3-0, zimepaa nafasi moja moja hadi nambari tisa na 10 kwa alama 42 sawa na Leopards, ambayo imeteremka kutoka nambari tisa hadi 11 kwa tofauti ya magoli. Nzoia, Western Stima na Rangers zimesalia katika nafasi 13, 14 na 15 kwa alama 38, 38 na 32 mtawalia.

Zoo imeruka Chemelil baada ya kuchapa Homeboyz 3-2 na kufikisha alama 31. Chemelil imevuna alama 31, huku Vihiga na Mount Kenya zikivuna alama 26 na 18 mtawalia.