Habari za Kitaifa

Cheo cha nuksi: Mikosi ilivyoandama manaibu rais Kenya tangu tupate uhuru

May 23rd, 2024 1 min read

NA MOSES NYAMORI

“SITARUHUSU naibu wangu kufedheheshwa jinsi manaibu wa rais wa zamani walivyodhalilishwa na jinsi nilivyodhalilishwa.”

Hayo yalikuwa maneno ya William Ruto wakati huo akiwa naibu rais katika mahojiano kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2022 alipokuwa akizozana na mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta.

Chini ya miaka miwili baada ya kuingia mamlakani, kuna manung’uniko ya uhusiano baridi kati ya Rais Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua. Baadhi ya washirika wa Bw Gachagua wamedai hadharani kuna njama ya kumzima ndani ya serikali.

“Sisi katika eneo la Mlima Kenya tuliamka asubuhi sana… tuliwachagua William Ruto na Rigathi Gachagua na tuliteseka sana katika mchakato huo. Nyote mnajua dhuluma alizofanyiwa Ruto alipokuwa naibu wa rais na hatutaruhusu haya yamfanyikie mwana wetu,” Gavana wa Nyeri Muathi Kahiga, mwandani wa karibu wa Naibu Rais, alidai Jumapili.

Lakini hii inaonekana kuwa kawaida ya kazi ya kuwa naibu wa rais Kenya.

Kuanzia Makamu wa kwanza wa Rais Jaramogi Oginga Odinga, hadi wengine kama Daniel Arap Moi, Joseph Murumbi, Dkt Josphat Karanja, Profesa George Saitoti na Dkt Ruto, ambaye alikuwa Naibu Rais wa kwanza, wote walipitia dhiki kuu na masaibu ya kisiasa, baadhi yaliyoanzishwa na wakubwa wao au vibaraka wa wakubwa wao.

Baadhi ya walioshikilia wadhifa huo walihujumiwa na kuondolewa ofisini.

Bw Gachagua anaonekana kushambuliwa, hasa na wanasiasa kutoka eneo lake la Mlima Kenya, ambao wanachukuliwa kuwa washirika wa karibu wa Rais Ruto.

Hao ni pamoja na Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru ambaye kwa sasa yuko pamoja na kiongozi wa nchi katika ziara yake ya Kiserikali Amerika, Waziri wa Utumishi wa Umma Moses Kuria na Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro. Hata hivyo, Bw Gachagua amewataja kama wasaliti wa eneo hilo.

Awali, rais alikuwa na mamlaka ya kuteua na kufuta kazi naibu wake kiholela.