Michezo

Chepkoech ahifadhi taji la Diamond League, avuna Sh5.1 milioni

August 30th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

BEATRICE Chepkoech alihifadhi ubingwa wake wa Riadha za Diamond League baada ya kushinda fainali ya mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji mnamo Agosti 29, 2019, mjini Zurich nchini Uswisi.

Katika makala hayo ya 10, mshikilizi huyu wa rekodi ya dunia ya mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji alitumia dakika 9:01.71 kubwaga washiriki 12 wakiwemo Wakenya wenzake Hyvin Kiyeng (9:03:83), Norah Jeruto (9:05:15) na Daisy Jepkemei (9:06.66) waliokamilisha mduara wa tano-bora.

Chepkoech, 28, ambaye ni bingwa wa Afrika, alijizolea Sh5,182,000 katika fainali. Alijishindia Sh1,036,400 anazopokea mshindi katika kila duru baada ya kubeba mataji ya Shanghai nchini Uchina (Mei 18), Stanford nchini Marekani (Juni 30) na Birmingham nchini Uingereza (Agosti 18).

Alifunga msimu juu ya jedwali kwa alama 39 akifuatiwa na Kiyeng (24), mshindi wa duru ya Olso Jeruto (21), Celliphine Chespol (19) na Jepkemei (16).

Waliomaliza msimu kutoka nafasi ya pili hadi nane walizawadiwa kati ya Sh2.0 milioni na Sh207,280 katika usanjari huo.

Washindi wote wa Zurich walifuzu kushiriki Riadha za Dunia zitakazofanyika jijini Doha nchini Qatar baadaye Septemba 2019.

Hii hapa orodha ya washindi wa kwanza 16 wa fainali mjini Zurich. Fainali ya pili itakuwa mjini Brussels mnamo Septemba 6.

Mabingwa wa fainali ya Zurich

Wanaume

Mita 100 – Noah Lyles (Marekani); Mita 800 – Donovan Brazier (Marekani); Mita 5000 – Joshua Cheptegei (Uganda); Mita 400 kuruka viunzi – Karsten Warholm (Norway); Kuruka kwa ufito – Sam Hendricks (Marekani); Kuruka Juu – Andriy Protsenko (Ukraine); Kuruka umbali – Juan Miguel Echevarria (Cuba); Kuruka mkuki – Magnus Kirt (Estonia)

Wanawake

Mita 200 – Shaunae Miller-Uibo (Bahamas); Mita 400 – Salwa Eid Naser (Bahrain); Mita 1500 – Sifan Hassan (Uholanzi); Mita 400 kuruka viunzi – Sydney McLaughlin (Marekani); Mita 3000 kuruka viunzi na maji – Beatrice Chepkoech (Kenya); ‘Triple Jump’ – Shanieka Ricketts (Jamaica); Kurusha mkuki – Lyu Huihui (Uchina); Kutupa tufe – Gong Lijiao (Uchina)