Michezo

Chepng’etich aibuka bingwa wa Dubai Marathon

January 25th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

RUTH Chepng’etich ameshindia Kenya taji lake la kwanza la Dubai Marathon baada ya ukame wa miaka 12 kwa kutimka muda wa kutisha katika nchi ya Milki za Kiarabu wa saa 2:17:07, Ijumaa.

Muda huu ni sekunde sita nje ya rekodi ya dunia inayoshikiliwa na Mkenya mwingine Mary Keitany.

Chepng’etich, ambaye atazawadiwa Sh10 milioni kwa ushindi wake, ni Mkenya wa pili katika historia ya miaka 20 ya mbio hizi baada ya Delilah Asiago kutwaa ubingwa wa Dubai Marathon mwaka 2006.

Chepng’etich, 25, ambaye alishinda Istanbul Marathon nchini Uturuki hapo Novemba 11 mwaka 2018 kwa muda wake bora wa saa 2:18:35, ni mwanariadha wa kwanza kukimbia umbali huu chini ya saa mbili na dakika 20 kwa kipindi kifupi (siku 75).

Mkenya huyu na Waethiopia Worknesh Edesa na Worknesh Degefa, ambaye alishinda Dubai Marathon mwaka 2017, walikamilisha kilomita 21 za kwanza pamoja.

Edesa aliachwa kati ya kilomita 25 na 30 kabla ya Chepng’etich kuchukua uongozi kabisa baada ya kilomita ya 35.

Chepng’etich sasa ni mkimbiaji wa tatu duniani mwanamke kutimka kasi ya juu baada ya Muingereza Paula Radcliffe (saa 2:15:25) na Keitany (2:17:01). Alifuta rekodi ya Dubai Marathon ya saa 2:19:17 ambayo Muethiopia Roza Dereje aliweka mwaka 2018.

Doa katika ushindi wa Chepng’etich ni kwamba yuko chini ya meneja Federico Rosa, ambaye wakimbiaji wake wengine Rita Jeptoo, Jemima Sumgong na Asbel Kiprop, walipatikana na hatia ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli za aina ya EPO. Degefa alikamilisha katika nafasi ya pili kwa saa 2:17:41 naye Edesa (2:21:05) akafunga tatu-bora.

Kwa mwaka wa nane mfululizo, Kenya haikushinda taji la wanaume, huku likienda Ethiopia tena kupitia kwa Getaneh Molla, ambaye pia alifuta rekodi ya Dubai Marathon ya saa 2:04:00 iliyoshikiliwa na mshindi wa mwaka 2018 Mosinet Geremew kutoka Ethiopia.

Molla alikamilisha umbali huo kwa rekodi mpya ya saa 2:03:34, ambayo ni kasi ya juu zaidi ya mkimbiaji anayeshiriki marathon kwa mara yake ya kwanza kabisa.

Waethiopia Lemi Berhanu na Guye Adola, ambao walikuwa katika orodha ya wakimbiaji waliopigiwa upatu kutamba, walijiuzulu naye Ibrahim Jeilan hakuanza. Herpassa Negasa na Asefa Mengstu walimaliza katika nafasi za pili na tatu kwa saa 2:03:40 na 2:04:24, mtawalia.